Tammy: Nitaibeba mikoba ya Kane England

Monday January 13 2020

Mwanaspoti-Tammy-Tanzania-Kane-England-Mwanasport-Michezo Leo-Michezo Habari-MWANASPORT

 

London, England. Mshambuliaji Tammy Abraham amesema yuko tayari kuvaa viatu vya Harry Kane katika fainali za Kombe la Ulaya.

Kane anaweza kukosa fainali hizo kwa kuwa amefanyiwa upasuaji wa mguu ambao unaweza kumuweka nje ya uwanja hadi Aprili, mwaka huu.

Abraham alisema amejiandaa kuchukua mikoba ya nahodha huyo wa England ikiwa atakosa fainali hizo.

Mshambuliaji huyo wa Chelsea amekuwa katika kiwango bora baada ya kufunga mabao 13 na Jumamosi alichangia ushindi wa mabao 3-0 iliyopata timu hiyo dhidi ya Burnley.

“Namuangalia Harry Kane, ameumia lakini naamini atarejea uwanjani kuzikabili fainali za Ulaya. Itakuwa fursa endapo atashindwa kupona kwa wakati,”alisema Abraham mwenye miaka 22.

Hata hivyo, alisema England ina idadi kubwa ya washambuliaji akiwataja Marcus Rashford, Jamie Vardy na Danny Ings ambao ni hodari wa kufunga mabao.

Advertisement

Abraham alisema anapenda kucheza England na anasubiri fursa kuitwa kuongoza kikosi hicho katika eneo la ushambuliaji ikiwa nyota huyo wa Tottenham Hotspurs atakosa fainali hizo.

Advertisement