Sven, Simba watua Dar es Salaam tabasamu kama lote

Muktasari:

Simba imefanikiwa kushinda mechi zake mbili dhidi ya Mbao na Alliance na kuendelea kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 41

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck amewasifu wachezaji wake kwa kupambana na kufanikiwa kupata pointi sita jijini Mwanza sasa akili yake kwa Mwadui.

Akizungumza baada ya timu yake kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere leo mchana wakitokea Mwanza, Sven alisema haikuwa safari rahisi kwao kwani walicheza mechi mbili katika mazingira magumu kutokana na kuwa na mvua nyingi.

Simba imefanikiwa kushinda mechi zake mbili dhidi ya Mbao na Alliance na kuendelea kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 41, huku ikifanikiwa kufuta machungu ya kipigo walichopata katika fainali ya Kombe la Mapinduzi kutoka kwa Mtibwa Sugar.

Kocha Sven alionekana kuwa mwenye furaha na kueleza safari hiyo ilikuwa yenye mafanikio kwao.

Sven alisema haikuwa safari rahisi kwani walicheza mechi mbili katika mazingira magumu baada ya kuwa na mvua nyingi mfululizo.

"Mvua hizo zilikuwa zinatupa changanoto katika uwanja haswa eneo la kuchezea halikuwa zuri kutokana na maji mengi yakiotuama," alisema.

"Nawapongeze wachezaji wangu wamenifurahisha kwa kazi ambayo wameifanya kwani kupambana na kujitolea kwao ndio wameifanya safari huu kuwa yenye mafanikio kwetu.

"Kupata pointi sita kwenye Uwanja CCM Kirumba si kazi rahisi, lakini hili ni moja ya mafanikio kwetu kwani ndio jambo ambalo tulilifuata.

"Nguvu na akili baada ya kurudi nyumbani tunaiweka katika mechi inayofuata ya Kombe la FA, dhidi ya Mwadui ili kupata ushindi pia," alisema Sven.