Winga wa Simba afichua wachezaji walivyohujumu viongozi

Muktasari:

Sunday anasema moja ya mambo ambayo yalikuwa ni kawaida kwenye kikosi cha Simba kufanyika ni wachezaji kushirikishwa katika matukio ya imani za kishirikina hasa wanapokaribia kucheza na Yanga.

Matukio ya viongozi hasa wa klabu kongwe za Simba na Yanga kung’olewa madarakani miaka ya nyuma hayakuwa mambo mageni, lakini nyuma ya mapinduzi hayo wachezaji wa klabu hizo walihusika.
Akizungumza nyota wa zamani wa Simba, Sunday Juma amefunguka namna wachezaji walivyotumika kuwang’oa viongozi na ahadi walizopewa endapo watafanikisha mbinu hiyo chafu.
Sunday au maarufu kwa jina la utani la ‘Pikipiki’ anasema mara nyingi mechi za Simba na Yanga ndizo zilitumika kuwang’oa viongozi.
“Walihujumiana wenyewe kwa wenyewe ndani ya klabu na sisi wachezaji walitutumia kuwahujumu kabla ya kufanya mapinduzi,” anasimulia Sunday.
Akitolea mfano moja ya mechi za Simba na Yanga baadhi ya Wanasimba walitaka kumpindua Jimmy Ngonya (aliyekuwa Katibu Mkuu).
“Baadhi ya wachezaji walifuatwa na kutakiwa kucheza chini ya kiwango tufungwe ile mechi ili Jimmy aundiwe zengwe aondoke,” anasimulia.
Anasema wazo hilo yeye Sunday hakuafikiana nalo, kwani katika mambo ambayo hakukubaliana nayo ni kuruhusu wafungwe kwa sababu ya maslahi ya mtu mwingine.
“Waliotushawishi walitaka baada ya mapinduzi mmojawapo ndiye achukue nafasi hiyo, lakini hawakuwa na mapenzi na klabu bali ni kwa maslahi yao binafsi, jambo ambalo sikuliafiki,” anafichua winga huyo.

Malipo kwa wachezaji
Sunday anasema wachezaji hawakuwa wakilipwa chochote zaidi ya ahadi ya kwamba wataendelea kubaki kwenye timu endapo yule aliyewashawishi kufungisha atafanikisha kumng’oa kiongozi aliyepo na yeye kuingia madarakani.
“Ile mechi tulishinda mabao 2-1 mimi ndiye nilifunga nikaonekana msaliti, lakini sikukubali kuingia katika mkumbo wa kufungisha ili mradi kiongozi aliyepo madarakani ang’olewe,” anasema.
Anasema baadhi ya wachezaji waliingia katika mkumbo huo bila kujua wanaowashawishi wanatafuta maslahi yao binafsi na si mapenzi ya klabu. Hiyo ilikuwa mwaka 1987.

Ushirikina
Sunday anasema moja ya mambo ambayo yalikuwa ni kawaida kwenye kikosi cha Simba kufanyika ni wachezaji kushirikishwa katika matukio ya imani za kishirikina hasa wanapokaribia kucheza na Yanga.
“Kuna siku tuligoma, tukawambia viongozi kama mnaona ushirikina unasaidia basi fanyeni nyie sisi wachezaji tuacheni tupumzike kwa ajili ya kusubiri mechi,” anasema Sunday.
Anasema walikuwa kambini kujiandaa na mechi na Yanga, uongozi ukawafuata na kuwataka wakasomewe dua usiku wa manane  kuamkia siku ya mechi hiyo.
“Tuligoma hakuna mchezaji aliyeamka kwenda tuliwambia wao wakasomewe kwa niaba yetu na sisi watuache tupumzike kusubiri mechi bila kuweka mgomo mtindo ungekuwa huo huo.
“Ilizoeleka tunaamshwa usiku badala ya kupumzika kusubiri mechi ndiyo kwanza mnakesha kwenye matukio ambayo hayafai tukiaminishwa kuwa tukifanya vile tutashinda jambo ambalo si kweli.
 “Zile zilikuwa ni imani tu, lakini kiuhalisia mambo yale hayasaidii lolote kwa kuwa tumejiaminisha hivyo  hata kama ikitokea mmepewa maji mkaambiwa ni dawa ya ushindi mtaamini wakati hakuna lolote,” anasema.

Jina la Pikipiki
Wengi wanamfahamu kwa jina la Pikipiki enzi akitamba na kikosi cha Simba, lakini jina hilo Sunday anasema lilianzia TPC ya Moshi.
Huku akicheka, Sunday anasema hakumbuki ni nani alimpa jina hilo, lakini alipachikwa hata kabla ya kutua Simba wakati huo akiwa Moshi.
 “Nilikuwa na kasi kwenye mechi nilikuwa nawambia tu wanitangulizie mpira mbele, hiyo ndiyo ilikuwa staili yangu, mabeki wengi walishindwa kwenda sambamba na kasi yangu huo ndio ukawa mwanzo wa jina la Pikipiki,” anasimulia.
Anasema kati ya timu zote alizocheza beki pekee ambaye alimmudu ni Ahmed Amasha wa Yanga, ambaye licha ya kwamba hakuwa na kasi, Sunday anasema alimdhibiti kwa kwa kutumia akili katika muda wote wa mchezo. “Alikuwa akiziba njia tu na akiwa karibu na mpira alikuwa na nguvu za ajabu humtoki kizembe ndiye alikuwa beki bora kwangu enzi nacheza mpira”, anasema nguli huyo.

Aliigomea Yanga
Sunday anakumbuka namna alivyoigomea Yanga ambayo ilimfuata mara mbili bila mafanikio na kwenda kucheza Simba bure.
“Nilikuwa na mapenzi na Simba tangu nikiwa shule ya msingi Mhanga, Singida enzi hizo shuleni tukicheza tunajigawa Yanga na Simba mapenzi yangu Simba yalianzia huko.
Anasema hata alipojiunga na timu ya BIT Kombaini na Kibo Shooting akiwa kwenye timu ya mkoa wa Kilimanjaro katika Kombe la Taifa alikuwa shabiki kindakindaki wa Simba.
Yanga walinifuata mara mbili na kunilipia tiketi, lakini niligoma kujiunga nayo nikisubiri ofa ya Simba baada ya Nico Njohole kuniambia klabu ina mpango huo.
Anasema baada ya muda kiongozi wa klabu hiyo, Alfred Sanga  alimfuata akiwa kwenye mashindano ya Shimuta Tanga na kumueleza mipango hiyo.
“Sikutaka kujivunga tuliweka mipango sawa ya nauli baada ya muda nikaja Dar es Salaam kuanza maisha mapya ndani ya klabu ya Simba mwishoni mwaka mwaka 1980.
Mbali na Sunday, nyota wengine waliojiunga naye kwenye usajili mpya ni Malota Soma, Thobias Nkoma, Amri Ibrahim, Zamoyoni Mogella, Innocent Haule na Ibrahim Malekano.
Anasema alicheza Simba kwa mapenzi na si maslahi, kwani hakulipwa chochote zaidi ya kuwa na mapenzi na klabu hiyo kongwe.

Manufaa
Tofauti na falsafa iliyojengeka kwa wachezaji kunufaika wakiwa katika viwango bora, kwa Sunday ilikuwa tofauti kwani baada ya kustaafu soka ndipo akapata mafanikio.
Sunday anasema alistaafu kwa heshima Simba mwaka 1990 na kufanyiwa sherehe ya kuagwa na kupewa zawadi mbalimbali ikiwa fedha Sh 100,000, feni, doti ya khanga na eneo la wazi kwenye jengo la Simba, Msimbazi Kariakoo kwa ajili ya kufanyia biashara.
“Eneo lile ndilo lilinipa mafanikio, kwani nilifanya biashara ya urembo wa kike ambayo ilinipunguzia ukali wa maisha na kuniwezesha kujenga nyumba Keko, Dar es Salaam.
Anasema alifanya biashara katika eneo hilo bure  kwa miaka mingi hadi klabu ilipojenga jengo jipya na kuwahamisha kwa makubaliano kwamba, ujenzi utakapokamilika watarejea.
“Baada ya ujenzi, uongozi uliokuwepo uligoma kuturudisha mimi na (alimtaja mchezaji mwingine wa Simba zamani), lakini kwa kipindi nilichokuwa pale nilifanikisha mambo mengi,” anasema.
Sunday ambaye  sasa ana duka la urembo wa kike Kariakoo jirani na yalipo makao makuu ya Simba anasema, kitendo cha klabu hiyo kumpa eneo la kufanyia biashara ni la pekee na linamfanya aendelee kuikumbuka mpaka sasa.

Azipa somo Simba, Yanga
Nyota huyo wa zamani aliyetokea Kibo Shooting na kujiunga na Simba anasema wachezaji wengi wanaotoka timu ndogo kujiunga na Simba au Yanga wengi wao huwa wanafeli kwa sababu ya uoga.
“Utakuta mchezaji ni mzuri ana kiwango bora, lakini akifika Simba au Yanga anaonekana hafai kwa sababu ya uoga na kutojiamini.
“Lakini ukiweka juhudi na kukubali kujifunza kila siku ni rahisi mno kuchezea hizo timu, tatizo wachezaji wengi hasa wa kizazi cha sasa hawajitumi na ikitokea amepangwa akaharibu na kuzomewa na mashabiki anakosa kujiamini na kila anachokifanya atakuwa anaona hawezi, jambo ambalo halitakiwi,” anasema Sunday ambaye alikuwa na kiwango bora cha kucheza nafasi ya winga wa pembeni.