Staa Genk amlilia Samatta akitimkia Aston Villa

Muktasari:

Samatta alitoa ahadi kuwa lazima atafute siku ya kwenda kuwaaga rasmi wachezaji wenzake hata baada ya kutambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa Aston Villa.

WINGA wa KRC Genk, Joseph Paintsil ambaye ni raia wa Ghana amesema kuondoka kwa Mbwana Samatta kwenye klabu hiyo ni pengo ambalo sio rahisi kuliziba kwa sababu mbali na uwezo wake wa kufunga alikuwa kiongozi.
Paintsil ambaye aliwahi kufichua kuwa Samatta ni rais wao ndani ya klabu hiyo mara ya mwisho tulipofanya naye mahojiano mwishoni mwa msimu uliopita, alisema atamkumbuka mshambuliaji huyo wa Tanzania kwa namna ya kipekee alivyompokea.
“Sam (Samatta) alinipokea hapa Genk, alikuwa kama kaka kwangu hadi nikawa mwenyeji, nilijisikia nipo nyumbani, alinisaidia kuimarika na tumekuwa tukiongea mengi hata masuala ya kimaisha kama vijana, ambao tumekuja Ulaya kutafuta.
“Alikuwa kiongozi akiwa uwanjani, tulikuwa tukijiamini zaidi akiwepo Samatta kwa sababu tulikuwa na imani muda wowote anaweza kufanya lolote, akiwa katika ubora wake hakuna wa kumzuia,” alisema nyota huyo wa Ghana.
Paintsil alisema kwa kiasi kikubwa Samatta alichangia kutwaa kwao ubingwa msimu uliopita, kwani  alikuwa akiwahamasisha chipukizi akiwemo yeye kucheza katika viwango bora - ndio maana ndoto ya kuchukua ubingwa ikawezekana.
Samatta aliachana na wachezaji wenzake nchini Ujeruman ambako KRC Genk iliweka kambi ya kujiandaa na michezo inayoendelea ya Ligi Kuu nchini Ubelgiji ambayo ilisimama kwa muda.
Kwa mujibu wa Paintsil, Samatta alitoa ahadi kuwa lazima atafute siku ya kwenda kuwaaga rasmi wachezaji wenzake hata baada ya kutambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa Aston Villa.
“Tutayaendeleza mazuri yake na kuhakikisha Genk inaendelea kufanya vizuri. Binafsi namtakia mafanikio mema, nitafurahi siku moja ikitokea nafasi ya kucheza naye tena timu moja,” alisema.