Staa Difaa Jadida: Kibabage anafuata nyayo za Marcelo wa Real Madrid

Muktasari:

Kibabage ameitwa katika kikosi hicho kwa ajili ya mashindano ya Chalenji yanayoandaliwa na nchi wanachama wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambayo yanayoanza kutimua vumbi Disemba 7 hadi 22, mwaka huu, kule Uganda

NAHODHA wa Difaa El Jadida, Youssef Aguerdoum ameifananisha staili ya uchezaji ya kinda la Kitanzania, Nickson Kibabage na beki wa kimataifa wa Brazil na klabu ya Real Madrid, Marcelo Vieira.
Aguerdoum, ambaye alikuwa akichezea Rachad Bernoussi kabla ya kujiunga na Difaa, alisema anapenda uchezaji wa Kibabage, ambaye ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya  Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’.
Kibabage ameitwa katika kikosi hicho kwa ajili ya mashindano ya Chalenji yanayoandaliwa na nchi wanachama wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambayo yanayoanza kutimua vumbi Disemba 7 hadi 22, mwaka huu, kule Uganda.
“Naweza kumfananisha na Marcelo, ni mzuri katika kushambulia, namuona mbali kama ataendelea kuwa msikivu na kupenda kujifunza. Nimekuwa nikifurahia kucheza naye,” alisema beki huyo wa kati.
Nyota huyo mwenye miaka 29, alisema utafika wakati wake kucheza hivyo hapaswi kuumizwa kichwa kuhusu kukosa nafasi ya kucheza.
“Bado ana umri sahihi kabisa na kwa uwezo wake umri wake ni mdogo pamoja na kuwa anauwezo mzuri, anatakiwa kujifunza zaidi kwa kuangalia wengine wanafanya nini.”
Katika kikosi cha kwanza cha Difaa, safu ya ulinzi imekuwa ikiongozwa na Aguerdoum  huku maeneo mengine wakicheza, Mohamed  El Yousfi, ambaye ni kipa, beki wa kulia ni Mehdi Karnass, beki wa kushoto, Ayoub Benchchaouil na Marouane Hadhoudi anayecheza kati na nahodha huyo.
Anayewania namba na Kibabage ambaye ni Benchchaouil, sio beki wa kushoto asilia, ni kiungo lakini amebadilishwa na kuanza kutumika kwenye eneo hilo kocha Zaki Badou.
Kibabage alikuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba katika mchezo wa Novemba 22 ambao, waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Raja Beni Mehllal huku Msuva akicheza kwa dakika 90 za mchezo huo.

ACHEKELEA KUITWA
Baada ya kuitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars, Kibabage amepata mzuka mpya na kufunguka kwamba, atatumia vyema nafasi hiyo ili kuipa Stars mafanikio.
“Kuitwa timu ya taifa ni jambo zuri kwangu kwa sababu ni kitu nilichokuwa nakitarajia. Nina mambo ya kujifunza huko,” alisema beki huyo wa kushoto wa zamani wa Mtibwa Sugar.
Kibabage, ambaye alikuwa sehemu ya wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya Taifa chini ya miaka 17 kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana za mwaka 2017 zilizofanyika nchini Gabon, pia aliwahi kuichezea timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20.