Masikini! Sonso ajifunga, kadi nyekundu Yanga yachapwa 1-0 Azam FC

Muktasari:

Hicho ni kipigo cha pili kwa Yanga wakiwa chini ya kocha Luc Eymael ambaye leo alipewa kadi njano na mwamuzi kutokana na kumtolea maneno makali.

Dar es Salaam. Bao la kujifunga la beki Ally Mtoni ‘Sonso’ pamoja na kupata kadi nyekundu vimetosha kuifanya Yanga kukubali kichapo 1-0 kutoka kwa Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliokuwa mgumu kutokana na mvua kubwa kucheza Yanga ilipata dakika 25, baada ya Sonso kujifunga mwenye wakati akijaribu kuokoa mpira wa kona kabla ya kupata kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumkanya kwa makusudi beki wa Azam, Nicolaus Wadada katika kipindi cha pili.

Hicho ni kipigo cha pili kwa Yanga wakiwa chini ya kocha Luc Eymael ambaye leo alipewa kadi njano na mwamuzi kutokana na kumtolea maneno makali.

Katika mchezo huo timu zote zilikuwa zinacheza mchezo wa kuviziana na kutumia mipira mirefu.

Mbinu hizo ilionekana kutumika vizuri na mabeki wa Yanga, Lamine Moro na Ally Mtoni kwani maumbo yao yaliwafanya wazuie vizuri mipira yote ya juu.

Dakika 10, David Molinga alikosa goli baada ya kupigiwa pasi na Mapinduzi Balama na kupiga shuti lilitoka pembezoni kidogo na uwanja.

Baada ya shambulizi hilo Azam walianza mpira kwa haraka kufanya shambulizi la kushtukiza kupitia mshambuliaji wao Shaban Chilunda.

Dakila 14 Azam waligongeana pasi za haraka haraka nje ya boksi na kiungo wao Salum Abubakari alikunjuka shuti ambalo lilipita karibu na mwamba wa chini.

Dakika 16 Yanga walitaka kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao Molinga baada ya kufanyiwa madhambi nje ya 18 na beki wa Azam, Daniel Amoah na kuwa faulo iliyopigwa moja kwa moja na Molinga ikagonga mwamba wa juu.

Katika mchezo huu Molinga aligeuka kuwa nyota kwa mashabiki wa Yanga kwani kila ambacho alikuwa akifanya.

Dakika 21 kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi alifyatuka shuti kali nje ya 18 akipokea pasi ya Mapinduzi Balama lakini mpira huo uliishia mikononi mwa kipa wa Azam, Razack Abarola.

Dakika 23 mshambuliaji wa Azam, Obrey Chirwa alipewa kadi ya njano baada ya kumkanyaga mguu beki wa Yanga, Jaffar Mohamed.

 

Azam ilipata bao dakika 25, mpira wa kocha uliopigwa na Bruce Kangwa ukapanguliwa na kipa wa Yanga, Faroukh Shikhalo na kwenda kumgonga gotini beki Sonso na kuingia wavuni.

Mabeki wa Yanga, Lamine Moro na Ally Mtoni walikuwa na kazi ya ziada kuhakikisha wanamzuia Obrey Chirwa ambaye alikuwa anawasumbua.

Kwa upande wa Azam mabeki wao Daniel Amoah na Oscar Masai walikuwa na kazi ya ziada kuhakikisha wanamzuia Molinga aliyekuwa katika kiwango bora.

Timu hizo zilikwenda mapumziko matokeo 1-0 kwa wenyeji Azam kuongoza. Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko dakika 56 kwa kumtoa Patrick Sibomana na kuingia Ditram Nchimbi.

Mabadiliko hayo yalionekana kupelela nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo alikuwa anacheza Molinga peke yake.

Azam nao walifanya mabadiliko dakika 67 kwa kumtoa Chirwa na kuingia Never Tigele kwenda kucheza katika eneo la kiungo mkabaji.

Azam walionekana kucheza kwa kujilinda na kuachana na mchezo wa kushambulia, hali ambayo ikawafanya wapinzani wao waanze kusogea golini.

Dakika 72, Deus Kaseke alifyatuka shuti kali nje ya 18 akipokea pasi ya Haruna Niyonzima na kupiga shuti kali ambalo lilimgonga beki wa Azam nakuwa kona isiyokuwa na faida.

Dakika 76 kiungo wa Azam, Raphael Bryson alipewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Ditram Nchimbi, wakati huo huo Yanga wakimtoa Mapinduzi Balama na kuingia Yikpe Gnamien na Azam wakimtoa Shaban Chilunda na kuingia Donald Ngoma.

Yanga ilipata pigo dakika 80, baada ya Sonso kupewa kadi nyekundu baada ya kumkanyaga beki Wadada ambaye alikuwa chini, hata hivyo Wadada ndio alionekana kuwa wa kwanza kumkanyaga mwenzake lakini tukio hilo halikuonekana na mwamuzi Hance Mabena.

Yanga walifanya mabadiliko dakika 88, kwa kumtoa Papy Tshishimbi na kuingia Said Makapu wakati huo Azam wakimtoa Idd Seleman na kuingia Masoud Abdallah.