Sofapaka yatema wachezaji watano

Muktasari:

Sofapaka maarufu Batoto ba Mungu imevunja ndoa yake na wachezaji hao wakiwamo Kasirye Mohamed, Philip Muchuma, Allan Katwe, Musa Mulunda na Isma Watenga baada ya kuonekana kukosa mchango wowote katika kikosi hicho.

NAIROBI, Kenya. KLABU ya Sofapaka FC imetema wanasoka watano huku ikipania kutwaa huduma za wanasoka wawili au watatu baada ya dirisha dogo la uhamisho kufunguliwa mapema mwezi ujao.
    Sofapaka FC iliyoshinda Ligi Kuu ya KPL mwaka 2009 imeachia wachezaji hao waliosajiliwa mapema msimu huu. 
     Hata hivyo, imesajili mnyakaji Nicholas Sebwato kutoka Bright Stars ya Uganda.
Sofapaka maarufu Batoto ba Mungu imevunja ndoa yake na wachezaji hao wakiwamo Kasirye Mohamed, Philip Muchuma, Allan Katwe, Musa Mulunda na Isma Watenga baada ya kuonekana kukosa mchango wowote katika kikosi hicho.
“Tunaendelea kupiga hatua kwenye kampeni zetu lakini bado hatujafaulu kufikia nafasi tunayolenga ambapo tunapania kusajili damu mpya katika mpango wa kukisuka kikosi chetu,’’ alisema kocha wa Sofapaka, John Baraza na kuongeza kuwa wanalenga kunasa huduma za beki, straika na kiungo ambapo tayari wametambua wanaotaka.
Kocha huyo aliyekuwa mchezaji wa zamani wa klabu hiyo alitwikwa jukumu hilo mwezi uliyopita baada ya kocha, Divaldo Alvez kupigwa kalamu. Tangu atwae mikoba hiyo ameongoza Sofapaka kushinda mechi nne na kutoka nguvu sawa mara moja.
Wanasoka hao wamevuna ushindi wa mechi tatu za mabao 2-1 kila moja mbele ya Wazito FC, Zoo Kericho pia Kisumu Allstars kisha kunasa bao 1-0 dhidi ya Mathare United kabla ya kuagana bao 1-1 na Kisumu Allstars.
Katika msimamo wa kipute hicho, Sofapaka FC inashikilia nane bora kwa alama 21 baada ya kushuka dimbani mara 13.