Simba kujiulizwa upya kwa Mbeya City, JKT Tanzania kwa Prisons hapatoshi leo

Muktasari:

Vinara hao wa ligi walitibuliwa rekodi yao ya kucheza mechi 12 bila kupoteza katikati ya wiki na Mwadui ya Shinyanga kwa kufungwa bao 1-0 katika mechi iliyokuwa ya 13 kwao tangu walipotunguliwa mara ya mwisho na Kagera Sugar, mechi ya ligi ya msimu uliopita iliyopigwa Mei 10.

Dar es Salaam. Ukizubaa imekuwa kwako ndiyo hali ilivyokuwa kwa sasa katika Ligi Kuu Bara, hiyo baada ya rekodi ya Simba ya kushinda mechi 12 mfululizo bila kupoteza kwa zaidi ya siku 170 kabla ya kukatwa stimu na Mwadui, huku Polisi Tanzania, Coastal Union nazo zikitoka kuuguza vipigo viwanja vya ugenini.

Simba leo Jumapili inaanza upya wakati watakapotaka kumaliza hasira zao kwa Mbeya City kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara wikiendi hii.

Vinara hao wa ligi walitibuliwa rekodi yao ya kucheza mechi 12 bila kupoteza katikati ya wiki na Mwadui ya Shinyanga kwa kufungwa bao 1-0 katika mechi iliyokuwa ya 13 kwao tangu walipotunguliwa mara ya mwisho na Kagera Sugar, mechi ya ligi ya msimu uliopita iliyopigwa Mei 10.

Hakuna ubishi matokeo ya mechi zilizopita za Ligi Kuu, yameongeza presha ya mechi za wikiendi hii na hata zile zikatazochezwa kesho Jumatatu, lakini kazi ipo kwa Mbeya City itakayokuwa wageni wa Simba iliyojeruhiwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mbeya City iliyotoka kuambulia suluhu dhidi ya Alliance, imekuwa tofauti na ile iliyozoeleka hasa walipopanda daraja msimu wa 2013-2014, ingawa kwa mechi zao mbili zilizopita wameonekana kuimarika kwa kiasi fulani kwani imevuna alama nne Kanda ya Ziwa.

Simba imekuwa na udhaifu wa mipira ya krosi na kona, huku pia safu yake ya ulinzi ikishindwa kuhimili kasi ya washambuliaji wa timu pinzani na kama hilo hawajalifanyia kazi, wanaweza kuwapa mwanya wageni wao Mbeya City kuwaadhibu kama ilivyotokea kwa Mwadui mjini Shinyanga.

Rekodi zinaonyesha Simba imekuwa wababe wa City tangu ilipopanda daraja, kwani katika mechi 12 walizokutana katika Ligi Kuu, Simba imeibuka na ushindi mara saba dhidi ya moja ya City na mechi tatu zikiisha kwa sare. Hata hivyo, kichapo kutoka kwa Mwadui ambayo walikuwa na historia nzuri ya kuwanyoosha, kimeonekana kuwapa hofu Simba waliotangaza kuingia na tahadhali kubwa katika mchezo wa leo.

“Ni kweli tuna rekodi nzuri dhidi ya Mbeya City, lakini hata Mwadui tulikuwa tunapata matokeo mazuri dhidi yao ila juzi tukapoteza hivyo kikubwa ni kutoidharau wapinzani wetu, ndio maana tumefanya maandalizi makubwa kwa ajili ya mechi hiyo ya Jumapili,” alisema Kocha Patrick Aussems wa Simba.

“Ligi imekuwa na ushindani na tunaamini mechi itakuwa ngumu, lakini mkakati wetu ni kuhakikisha tunarudi kwenye kasi yetu ya ushindi iliyotibuliwa na matokeo tuliyopata dhidi ya Mwadui,” aliongeza.

Upande wa Mbeya, Kocha Mkuu wake aliyeipandisha timu hiyo, Juma Mwambusi alitamba watapambana kwa kila njia kuona wanapata ushindi ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya klabu 20.

Simba itaishukia Mbeya ikiwa na mzuka baada ya baadhi ya nyota wake waliokuwa majeruhi kama Mohammed Tshabalala, Shomary Kapombe wakirejea, lakini hata wapinzani wao baadhi ya wakali wake kuonekana tishio msimu huu, hasa mkongwe Peter Mapunda mwenye mabao manne.

Ukiondoa mechi ya Simba, leo pia kuna mchezo mwingine unaotarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu wakati JKT Tanzania itaikaribisha Prisons na kuna sababu tatu za kuufanya ufuatiliwe zaidi.

Kwanza ni upinzani wao wa jadi baina ya timu hizo kutokana na kumilikiwa na Vikosi vya Majeshi ya Ulinzi na Usalama, wenyeji  wakiwa chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati Prisons inamilikiwa na Jeshi la Magereza.

Pia timu hizo zimepishana kwa pointi moja tu katika msimamo, JKT ikiwa nafasi ya sita na pointi 12, moja zaidi na ilizonazo Prisons wenye alama 11.

Kingine ni hamu ya JKT kutaka kuvunja rekodi ya Prisons ya kutopoteza mchezo wowote Ligi Kuu, ikiwa timu pekee mpaka sasa kwani vigogo Simba, Yanga na Azam zote zimeshatobolewa.

Beki wa Prisons, Salum Kimenya aliliambia Mwanaspoti mbali na kulinda rekodi yao ya kupoteza, hesabu yao kubwa ni kumaliza ligi katika nafasi nzuri ndani ya msimamo wa ligi.

“Mechi zetu dhidi ya JKT siku zote zimekuwa ni ngumu na ukizingatia kocha wao alishawahi kutufundisha. Kwa upande wetu tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata ushindi katika kipindi hiki ili pale ligi itakapochanganya tuwe katika nafasi nzuri,” alisema.

Huko Mtwara, baada ya mechi zao mbili dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United kuahirishwa kutokana na ajali waliyopata siku kadhaa zilizopita, Ndanda inarejea uwanjani ikiialika Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona. Ushindi wa ugenini utaifanya Ruvu isogee hadi nafasi ya pili katika msimamo kwani itafikisha pointi 18, ila kwa Ndanda, wanahitaji ushindi ili waondoke nafasi ya pili kutoka mkiani waliopo kwa sasa wakiwa na pointi nne.

Huko Mkwakwani Tanga, Wagosi Coastal Union waliopo nafasi ya tisa watakuwa na kazi ya kufuta machungu ya kipigo cha mabao 2-0 walichokipata ugenini dhidi ya Mtibwa katika mchezo uliopita watakapoialika Mbao iliyotoka kupata sare ya 1-1 na Prisons katikati ya wiki.

Kadhalika Uwanja wa Ushirika Moshi kuna utamu mwingine wakati Polisi Tanzania itaialika Alliance, huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza 2-0 mechi iliyopita ugenini dhidi ya Lipuli.  Ushindi wowote leo utaifanya Polisi iliyopanda msimu huu sambamba na Namungo ya Lindi itaifanya ifikishe pointi 13 zinazoweza kuwaogeza kuingia Tano Bora kutoka nafasi ya 12 waliopo sasa.

Hata hivyo, haiwezi kuwa kazi rahisi kwao, kwani Alliance nao itakuwa ikisaka ushindi ili ifikishe alama 14 na kutinga Nne Bora iliyotawaliwa na Simba, Kagera Sugar, Ruvu Shooting na Namungo (kabla ya mechi za jana Jumamosi). Kocha wa Alliance, Kessy Mziray alisema hana wasiwasi wa kuikabili Polisi ugenini, licha ya kukiri utakuwa mchezo mgumu.

“Mechi itakuwa ngumu lakini faida ya kuuzoea uwanja wa Ushiriki nadhani itakuwa chachu ya kutupatia ushindi. Vijana wako tayari kwa mchezo na wanafahamu umuhimu wa kupata ushindi katika mechi hiyo,” alisema Mziray.