Simba kuvuna Sh1.2 Bilioni usajili wa Samatta wa Aston Villa

Muktasari:

Simba inaendelea kujivunia uamuzi wa kumuuza Samatta kwenda TP Mazembe ambako, aligeuka kuwa staa mkubwa kabla ya kuuzwa Genk ya Ubelgiji ambako, nako jina lake linaimbwa na mashabiki kwa kazi kubwa ya kupasia nyavuni.

WAKATI Watanzania wakipagawa na usajili wa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwenda Aston Villa ya Ligi Kuu England, Simba wenyewe wanachekelea kupiga pesa ndefu kupitia mauzo hayo.
Samatta jana jioni alitarajiwa kukamilisha dili lake la Pauni 8.7 (Zaidi ys Sh 27 bilioni) kwenda Aston Villa akitokea Genk ya Ubelgiji, Simba wenyewe wanajiandaa kufuatilia mgawo wao wa asilimia tano kwenye mauzo hayo kama taratibu za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) livayoelekeza.
Simba inaendelea kujivunia uamuzi wa kumuuza Samatta kwenda TP Mazembe ambako, aligeuka kuwa staa mkubwa kabla ya kuuzwa Genk ya Ubelgiji ambako, nako jina lake linaimbwa na mashabiki kwa kazi kubwa ya kupasia nyavuni.
Wakala wa mchezaji huyo, Jamal Kasongo alisema kwa mujibu wa kanuni kila klabu alikopita Samatta inapaswa kupata mgao huo ikiwemo Simba ambayo aliichezea kabla ya kutua TP Mazembe ya DR Congo na baadaye Genk. Samatta pia aliwahi kukipiga African Lyon na Mbagala Market zote za Dar es Salaam.
Alisema mgao huo unategemea na muda aliokaa kwenye klabu hizo pamoja na klabu iliyomlea kisoka.
“Mgao wa klabu ni asilimia tano, zitagawaje hapo ndipo haijajulikana lakini kote alikopitia zinapaswa kupata kwa mujibu wa kipengele cha Solidarity Contribution kwenye kanuni za Fifa,” alisema Kasongo.
Alisema hata alipouzwa kutoka TP Mazembe kwenda Genk, Simba ilipewa mgao huo ambao alisema kwa mujibu wa mkataba wake wakati akiuzwa Mazembe, Simba ilipewa Euro 100,000.

Simba wafunguka
Aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba, ambaye sasa ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah (Try Again) alisema bado hawajafahamu kiasi halisi cha mgao wa Simba baada ya Samatta kuuzwa Aston Villa.
“Inabidi kufuatilia, lakini hata alipouzwa Genk tulipaswa kupewa euro 100,000, lakini Mazembe walitupatia dola 50,000 pekee,” alisema Try Again na kuongeza.
“Mazembe walifanya uhuni, lakini bado hatujachelewa wakati tunafuatiliamgao wa Aston Villa kwa sababu ni haki ya Simba,” alisema.

Rage apigilia msumari
Aliyewahi kuwa rais wa Simba, Ismail Rage ambaye ndiye alimuuza Samatta, TP Mazembe alisema wakati wakimuuza katika ibara ya tano ya mkataba wake, walisema endapo mchezaji huyo atauzwa mahala pengine popote Simba itapata asilimia 20 ya malipo.
“Sijui kama mkataba ulichezewa, alipouzwa kwenda Genk niliwakumbusha Simba juu ya hilo, lakini pia hata kipindi hiki anapokwenda Aston Villa ni muhimu kufuatilia ili kupata mgawo wanaostahili,” alisema Rage.
Alisema fedha hizo haziwezi kuwafikia Simba kienyeji, lazima wafuate taratibu na kuambatanisha vithibitisho vinavyoenyesha madai yao ni halali ikiwamo kopi ya mkataba.
Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa Simba inaweza kuvuna zaidi ya Sh 1 bilioni ikiwa ni mgawo wa mauzo hayo.