Simba SC kumenoga Matola kumng'oa Kitambi

Muktasari:

Uongozi wa Polisi Tanzania, umekiri ishu ya Matola kwenda Simba imekamilika baada ya kumalizana na mabosi wenzao na kama mambo yakienda vizuri kocha huyo leo Jumatatu atakabidhi ofisi na kuaga rasmi ili kwenda zake Msimbazi.

KWA sasa zinahesabika saa tu kabla ya Kocha Seleman Matola kutua Msimbazi, baada ya mabosi wa Polisi Tanzania kumalizana na wenzao wa Simba. Lakini, kuna taarifa mbaya kwamba, Kocha Msaidizi wa Wekundu hao, Dennis Kitambi naye yupo mbioni kutemwa klabuni hapo.
Juzi Jumamosi kwenye taarifa yao ya kumtimua aliyekuwa Kocha Mkuu wao, Patrick Aussems, Simba ilisema Kitambi atakuwa Kaimu Kocha Mkuu wakati mchakato wa kocha mpya ukifanyika, lakini habari zilizopenyezwa kwa Mwanaspoti ni kwamba, hata yeye hana maisha marefu.
Habari hizo za ndani zinasema kuwa, Kitambi naye atapewa mkono wa kwaheri na nafasi yake itachukuliwa na Matola, ambaye kila kitu juu ya kurejea kwenye klabu yake hiyo ya zamani aliyowahi kuichezea na kuinoa kwa vipindi tofauti, kimekamilika na anasubiriwa kutambulishwa tu.
“Suala la Matola kwa sasa limekamilika, ndiye atakayekuja kuchukua nafasi ya Kitambi, kwani hata yeye ataachwa, huku mchakato wa kupata kocha mpya mapema kabla ya mechi yetu ya watani ukiendelea,” kilisema chanzo hicho.
Awali, ilielezwa kuwa Kitambi angebakishwa kikosini ili kusaidiana na Matola chini ya kocha ajaye, lakini mabosi wa Simba ni kama wamebadilisha mawazo na kutaka Matola asalie pekee yake na kulifumua benchi nzima la Aussems, ambaye aliwapa taji la pili mfululizo la Ligi Kuu.

POLISI KIROHO SAFI
Uongozi wa Polisi Tanzania, umekiri ishu ya Matola kwenda Simba imekamilika baada ya kumalizana na mabosi wenzao na kama mambo yakienda vizuri kocha huyo leo Jumatatu atakabidhi ofisi na kuaga rasmi ili kwenda zake Msimbazi.
Makamu Mwenyekiti wa Polisi, Robert Munisi alisema uongozi wao ulipokea barua kutoka Simba ya kumuomba Matola na halikuwapa tatizo kwao baada ya kukaa mezani na kumalizana na Matola.
“Tulikutana mwishoni mwa wiki na Matola pamoja na uongozi wa Simba baada ya kupokea barua yao, kwa sasa kila kitu kimekwenda safi na kilichobaki ni Matola kuvunja mkataba kama unavyoeleza hata sasa. Upande wetu hatuna tatizo na Simba wala kocha, yote ni kheri kuona mtu anapata mafanikio zaidi kwenye kazi yake.
“Kwa sasa nipo njiani natoka Dodoma nilipokwenda kukutana na uongozi, hivyo kesho (leo) Jumatatu tutamaliza taratibu zote kuhusu Matola na timu itakuwa chini ya Ali Suleiman Mtuli aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi hadi pale tutakapokamilisha zoezi la kumpata kocha wa kuziba nafasi hapo baadaye,” alisema.
Alisema wanachosubiri ni Matola kuweka mezani fedha za kuvunja mkataba kama walivyokubaliana wakati wakimchukua kuiongoza timu hiyo Juni mwaka huu, kwa kulipa mara tatu ya mshahara wake aliokuwa akiupokea.
“Siwezi kukwambia kiasi ambacho anatakiwa kukilipa labda yeye akuambie alikuwa analipwa kiasi gani na uzidishe mara tatu nadhani utakuwa umepata jibu ni kiasi gani atailipa Polisi Tanzania.
“Suala hili limekuwa faraja kwetu kwa kuondoka kocha kwa amani bila ugomvi na muda wowote anaweza kurejea maana tumemalizana kiutu uzima na haya ni maisha kuna leo na kesho. Lazima vitu vibadilike na watu watambue hadi kocha anaondoka kulikuwa hakuna tatizo lolote ndio maana tumemwachia na hata wachezaji kwa wachezaji wakifuata utaratibu tutawaachia,” alisema.
Matola mwenyewe alipotafutwa jana alisema kwa kifupi na kukata simu; “Niache kwanza nitakupigia baadaye tuongee vizuri.”
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alipoulizwa kuhusu taarifa za Kitambi kupishana na Matola Msimbazi, alipotezea na kudai hizo ni taarifa tu hata yeye anazisikia tu.
“Sijui lolote kwa kweli, kama kutakuwa na taarifa yoyote mtajulishwa, lakini kwa sasa ni kwamba Simba imeachana na Aussems na timu ipo chini ya Kitambi wakati tukitafuta kocha mwingine wa kuendelea kuingoza Simba kufikia malengo yake,” alisema Mazingisa.