Simba SC v Mtibwa Sugar: Huku Kibaya kule Kagere mnapigwa

Muktasari:

Pambano la Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2020 linalozikutanisha Mtibwa Sugar na Simba, litapigwa kuanzia saa 2:15 usiku kwa ajili ya kupata bingwa mpya baada ya waliokuwa wanalishikilia Azam FC wakitemeshwa mzigo kwenye hatua nusu fainali.

Zanzibar. HAPA Zenji buana hakuna siku muhimu na inayotukuzwa kama Sherehe za Mapinduzi ambazo huanzia katika mkesha wa kuamkia Januari 12, unaambiwa kuanzia usiku wa saa sita ya kuamkia siku hiyo kunakuwa na vurugu za sherehe hizo.
Si mnajua jana Jumapili ilikuwa kilele cha kumbukizi hiyo muhimu kwa Visiwa vya Zanzibar, ila sasa kwenye Uwanja uleule wa Amaan mjini hapa asubuhi ya jana kulikuwa na pilikapilika za maadhimisho ya Miaka 56 jana, usiku leo utakuwa na kazi nyingine nzito.
Lile pambano la Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2020 linalozikutanisha Mtibwa Sugar na Simba, litapigwa kuanzia saa 2:15 usiku kwa ajili ya kupata bingwa mpya baada ya waliokuwa wanalishikilia Azam FC wakitemeshwa mzigo kwenye hatua nusu fainali.
Pambano hilo ni kama marudio ya mechi za fainali za mwaka za 2008 na 2015 wakati timu hizo zilipokutana na Wekundu wa Msimbazi kutakata mara zote na kubeba taji la michuano hiyo, hivyo leo Mtibwa itakuwa ikisaka kulipa kisasi na wenzao wakitaka kuendeleza ubabe wao kwao.
Kwa aina ya vikosi vilivyochezeshwa kwenye michuano hiyo na aina ya mbinu za timu zote, bila ya shaka mashabiki wa soka watapata burudani na dakika 90 zinaweza kuamua bingwa kwani yoyote atakayezubaa lazima ile kwake na kumwachia mwenzake anyakua ubingwa huo wa msimu wa 14.
Utamu ni kwamba timu zote zimetinga hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti tena wakiving’oa vigogo wa soka, Simba iliivua taji na kuitupa nje Azam wanaoshikilia rekodi ya kubeba kombe hilo mara tano na Mtibwa wakiing’oa Yanga pia kwa matuta baada ya dakika zao 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mtibwa ndio iliyokuwa ya kwanza kwa kuifunga Yanga penalti 4-2, kisha siku inayofuata Simba kushinda kwa mikwaju 3-2 baada ya dakika zao 90 na Azam kumalizika kwa suluhu.
Kikosi cha Mtibwa chini ya kocha mzawa, Zuberi Katwila juzi kilifanya mazoezi yake ya mwisho katika Uwanja wa Mau Tse Tung, lakini jana wakapumzika kusubiri mchezo huo, huku wachezaji wakionekana kuwa na ari ya kutaka kulipa kisasi mbele ya vinara hao wa Ligi Kuu Bara.
Mwaka 2008 Mtibwa ilitunguliwa bao 1-0 na Simba kisha kuja kupasuka tena kwa penalti 4-3 mwaka 2015 na kuwapa Simba taji lao la tatu na la mwisho kwenye michuano hiyo, huku wenyewe (Mtibwa) ikiwa imetwaa mara moja tu mwaka 2010 licha ya kucheza fainali tano tofauti na kutoka kapa.
Kocha Katwila alikiri mchezo wa leo utakuwa mgumu na utaamuliwa na ufundi na mbinu, sambamba na namna wachezaji watakavyojitoa uwanjani, lakini kiu yao ni kutaka kubeba taji kwa mara ya pili kwani wamechoka kuwa daraja la kila wafikapo fainali kuwapa wapinzani wao ubingwa.
Alisema ameiona Simba ikiumana na Azam na sasa anajua kila mbinu za wapi wanapata nguvu ya kuwa bora na tayari wameshajipanga kuwadhibiti.
“Tunakutana na Simba, tukijua ubora wao, kwani licha ya kufika fainali pia kule nyumbani ndio vinara wa ligi, sio timu nyepesi na pia walichatufunga katika fainali mbili tulizowahi kukutana nao, japo hata sisi tulishawafunga kwenye hatua nyingine za michuano hii ya Mapinduzi,” alisema Katwila.
“Hii ni mechi ya fainali ambayo lazima mshindi apatikane kikosi changu kipo tayari kwa vita hii, vijana wangu tumewapa mbinu za jinsi gani kuweza kuwadhibiti wapinzani wetu na kufanikiwa kushinda.”
Upande wa Simba naoambao baada ya kuupiga mpira mwingi katika mchezo wa nusu fainali na kuizima Azam wametamka hawatafanya makosa kama waliyoyafanya watani wao Yanga mbele ya Mtibwa ambao wamekiri sio timu ya kubezwa japo waliichapa katika Ligi mabao 2-1.
Kocha Msaidizi, Seleman Matola alisema hawamdharau yeyote na mbele ya Mtibwa watashuka uwanjani wakiwa kamili kuhakikisha wanachukua taji hilo kwa mara ya nne.
Licha ya kukosekana mastaa wao kadhaa kama Deo Kanda, Clatous Chama lakini bado wana jeuri kwa vile kikosi chao kikafanya kweli na kufanikiwa kuibana Azam.
Matola alisema kuwa watapanga mziki mzito kuweza kulisaka taji lao hilo la kwanza kwa mwaka huu ili kuwapa furaha ambayo mashabiki wao wanataka.
Alisema wataingia katika mchezo huo wakiwa na mbinu zote katika kuisuka ushindi ndani ya dakika 90 lakini hata kama itashindikana wana ubora wa kuchukua kombe hata kwenye matuta.
“Mtibwa sio timu ya kuidharau kama mnavyoona wamewatoa Yanga na hii ni fainali. Kila timu ina nafasi yake muhimu ni maandalizi yenu, tuko tayari na tumekiandaa kikosi vyema kwa kucheza fainali na sio kingine tunataka kuchukua taji hili kuendelea kuweka rekodi bora katika mashindano haya.”
Timu zote zinajivunia wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa kisoka ambao tangu kuanza kwa michuano ya msimu wameonyesha kwanini timu zao zilifika fainali, huku Mtibwa wakibebwa na rekodi za kupenya kila hatua kwa matuta kwani kabla ya kuing’oa Yanga waliichapa Chipukizi kwa penalti 4-2 baada ya kumaliza dakika 90 bila kufunga, hivyo Simba wajipange inafika kwenye matatu.