Simba 2-0 Mbeya City: Kagere apiga bao la nane, Chama kawa mtamu

Muktasari:

Katika mchezo huo Kocha wa Simba, Patrick Aussems amewaanzisha washambuliaji watatu, Miraji, Kagere na Ibrahim Ajibu katika kuhakikisha Simba inapata ushindi.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Meddie Kagere amefunga bao lake la nane kwa mkwaju wa penalti na Clatous Chama kuifanya Simba kuongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City hadi mapumziko kwenye Uwanja wa Uhuru.

Kagere alifunga bao hilo dakika 8, baada ya mshambuliaji Miraj Athumani kuchezewa faulo katika eneo la penalti baada ya kumpiga chenga beki wakati anapiga shuti alichomekewa kwa nyuma.

Kiungo Chama alifunga bao la pili kwa Simba katika dakika 42, akipiga shuti kali akiwa umbali wa mita 18 na kumwacha kipa wa Mbeya City akiruka bila ya matumaini.

Katika kipindi cha kwanza cha mchezo, kipa wa Mbeya City, Richard Peter alifanya kazi nzuri kwa kuokoa hatari zilizokuwa zinaelekea langoni mwake dhidi ya washambuliaji wa Simba iliyokuwa ikiongozwa na Kagere.

Katika mchezo huo Kocha wa Simba, Patrick Aussems aliingia na mfumo wa 4-3-3 akiwaanzisha washambuliaji watatu, Miraji, Kagere na Ibrahim Ajibu katika kuhakikisha Simba inapata ushindi mnono.

Simba imeingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa 1-0 na Mwadui na kuharibu rekodi yao ya ushindi wa mechi sita za mwanzo wa Ligi Kuu Tanzania.

Miraj ameifungia timu hiyo mabao manne, ameanza katika safu ya ushambuliaji akiwa na kinara wa mabao katika Ligi hiyo, Meddie Kagere (8).

Mbali na Miraji, katika kikosi cha wekundu wa Msimbazi, kilichoanza dhidi ya Mbeya City, wameonekana kurejea, Mohammed Hussein 'Tshabala' na Shomary Kapombe waliokuwa majeruhi.

Aliyeanza katika golini ni Aishi Manula, mabeki wa pembeni ni Kapombe na Tshabalala huku upande wa kati wakianza, Pascal Wawa na Erasto Nyoni.

Katika eneo la kiungo, wameanza Mzamiru Yassin,Clatous Chama, Sharaf Shiboub na Ibrahim Ajibu. Washambuliaji ni Miraji na Kagere.

Kikosi cha Mbeya City kinaundwa na Richard Pater, Said Gamba, Bakar Ngusa, Ally Lundenga, Samson Madeleke, Mangoma Seleman, Pater Mapunda, Haroun Mandanda, Keneth Kinambi na Mpoki Mwakinyuke.

Tanga: Uwanja wa Mkwakwani; Wenyeji Coastal Union ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 25, kupitia Shaaban Dudu na sasa wanaongoza kwa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC.