Sheria kuamua ishu ya Mkwabi kuondoka Simba SC

Muktasari:

Hadi sasa nafasi yake haijajazwa na kwa mujibu wa katiba ya sasa ya klabu hiyo haijaeleza utaratibu wa kumpata mwenyekiti mpya endapo wa zamani atajiuzulu ama kuondolewa madarakani

Dar es Salaam. NI miezi miwili sasa tangu Mwanachama wa Simba, Swedy Mkwabi alipojiuzulu nafasi ya mwenyekiti wa klabu hiyo namchakato wa kuziba nafsi yake sasa utaamuliwa na wanasheria wa klabu hiyo.
Mkwabi alijiuzulu nafasi hiyo Septemba mwaka huu ikiwa hajamaliza hata mwaka madarakani tangu achaguliwe Novemba mwaka jana.
Hadi sasa nafasi yake haijajazwa na kwa mujibu wa katiba ya sasa ya klabu hiyo haijaeleza utaratibu wa kumpata mwenyekiti mpya endapo wa zamani atajiuzulu ama kuondolewa madarakani.
Awali kabla Simba haijabadilisha katiba yake ilielezwa kiongozi anapojiuzulu ama kupatwa na tatizo litakalomuweka kando kwenye nafasi hiyo, basi nafasi yake itakaimiwa na mjumbe mwenye uzoefu kuliko wajumbe wengine wote kwa wakati huo uchaguzi utafanyika ndani ya miezi mitatu.
Katiba ya sasa, sehemu ya tatu B Ibara ya 29 inayozungumzia muundo, inasema Klabu ya Simba itafanya kazi chini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Simba Sports Club Company Limited, kwa maana hiyo uamuzi wa kufanya uchaguzi kuziba nafasi ya Mkwabi utaamuliwa na bodi hiyo pasipo kujali ni muda gani.
Awali, Simba maamuzi mengi ya klabu yalikuwa yakiamuliwa na wanachama kwa kuitisha mkutano mkuu wa mwaka ama wa dharura kujadili jambo husika kwa wakati huo.
Kwa sasa, Simba itafanya Mkutano Mkuu wa mwaka, Desemba 8 mwaka huu ambapo utajadili mambo mbalimbali ingawa ajenda bado hazijawekwa wazi.
Habari zaidi zinasema kwa sababu Katiba ya Simba imenyamaza bila kueleza lolote, basi suala hilo la Mkwabi sasa litaamuliwa na wanasheria wa Simba.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Ngh’ambi ameliambia Mwanaspoti: “Kama Katiba haijaeleza kitu basi kuna wanasheria wa Simba ambao watakaa kuona ni jinsi gani mwenyekiti atapatikana.”
Kuhusu Mkutano Mkuu, Mulamu alisema: “Ni  wa kila mwaka kwa mujibu wa Katiba ya Simba, hivyo ajenda ni za kawaida za kujadili ndani ya Simba.”