Samatta apiga bao, Genk yachezea kichapo

Muktasari:

Samatta ataiongoza KRC Genk keshokutwa Jumanne kucheza mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Antwerp.

LICHA ya kutimuliwa kwa Felice Mazzu, KRC Genk anayoichezea nahodha wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta imeendelea kufanya vibaya katika Ligi Kuu Ubelgiji wakipoteza mchezo wanne mfululizo.

Genk wakiwa nyumbani wamekumbana na kipigo mabao 2-1 kutoka kwa Sint-Truiden jana Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji.

Katika mchezo huo, Genk ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya tisa ya  mchezo kupitia kwa  Samatta likiwa ni goli lake la saba msimu huu katika  michezo 16 wa Ligi Kuu  Ubelgiji.

Sint-Truiden walisawazisha ndani ya dakika hizo 45 za kipindi cha kwanza. Kipigo hicho cha Genk inaendelea kuwaondoa taratibu katika mstari wa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Jupiler Pro.

KRC Genk tangu wamtupishe virago vyake Felice Mazzu na nafasi yake akachukua Hannes Wolf, wameshindwa kuibuka na ushindi wa mchezo hata mmoja katika mshindano yote.

Walianza kupoteza kwa mabao 2-0, Novemba 10 dhidi ya Gent, Novemba 23 wakatoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Royal Excel Mouscron, Novemba 27 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya wakafungwa na Salzburg kwa mabao 4-1 huku mchezo wao wa mwisho kucheza ukiwa dhidi ya Sint-Truiden.

Wolf ambaye ni kocha wa zamani wa Mario Gotze anamtiani mwingine keshokutwa, Jumanne wa kuiongoza KRC Genk kucheza mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Antwerp.

Philippe Clement ambaye aliipa mafanikio timu hiyo msimu uliopita ambao walitwaa Jupiler Pro aliamua kuachana na klabu hiyo mwishoni mwa msimu kwa lengo la kwenda kwingine kukabiliana na changamoto mpya za soka.