Gozi la Ng'ombe: Samatta anatabasamu, Simba wameenda chini ya mbuyu

Muktasari:

Ndipo hapa ambapo naiona sura ya Mbwana Samatta. Pamoja na njaa ya Samatta bado maisha ya TP Mazembe yalikuwa ndio njia yake kuu. Kuishi na kupendwa na Moise Katumbi Chapwe ilikuwa ni jambo bora na alipata mwanga wa kibiashara na namna ya kuishi kifalme.

Kwenye uhalisia wa jua linalozama Magharibi baada ya kuibuka Mashariki, Tanzania imeshuhudia mambo machache ya kujivunia katika michezo. Tangu kipindi cha mzee Akwari, kisha akina Filbert Bayi au ile historia ya Leodegar Tenga na Afcon ya mwaka 1980 mpaka kwa Hasheem Thabeet ndani ya NBA na mwaka 2019 tulipofika katika Fainali za Afrika kule nchini Misri.
Mara nyingi tumeona jua linalochomoza lakini mara nyingi tumeshindwa kufuatilia linapokwenda kuzama kwa sababu tunakuwa tumefurahia mwanga vya kutosha na hatuna mpango wa kufahamu kuwa jioni kuna nyota na mwezi ambavyo vinapendezesha ulimwengu vyema zaidi.
Hakuna anayejishughulisha na kurejea kwa Shabani Chilunda kama ambavyo hakuna aliyejali maisha ya Lunyamila kipindi ambapo aliposemekana amepata nafasi nchini Ujerumani.
Mipango mingi imekuwa ya ujanja ujanja na ndio maana hata leo ninapoandika makala hii tunaishi na Shomari Kapombe alifika Ufaransa na hana kumbukumbu ya mnara maarufu wa Eiffel yaani hakuwa na njaa ya kubaki huko kwa sababu hakuwa na watu sahihi wa kumuelekeza .
Kila nikiwaza kwanini mara zote tunawaonea wivu watu wa nchi za Afrika ya Magharibi nakumbuka pia kuwa wenzetu wanaishi kwa malengo, wanaishi kwa tama, wanaishi kwa nia ya Sadio Mane ya kutoroka nyumbani ili siku moja aje kujenga msikiti, shule na hospitali kwenye kijiji alikozaliwa.
Lakini kwanini watu wenye msukumo huu wanafanikiwa kwa wenzetu? Sababu ni moja tu kuna walafi ambao hawajajaliwa vipaji kwenye miguu yao lakini wanajua namna ya kuifikisha miguu yenye vipaji mbali kwa sababu hapa ndipo fedha yao ya kula itakapopatikana ama kama wazungu wanavyoita “win win situation”.
Kila nikiorodhesha nikiorodhesha majina napata hisia kabisa kuwa tatizo la wachezaji wetu kutokufanikiwa halianzii kwao bali linaanzia kwa wawezeshaji wao au wasimamizi ambao wanatakiwa kuwa na ndoto sawa au zaidi ya wachezaji hawa.
Ndipo hapa ambapo naiona sura ya Mbwana Samatta. Pamoja na njaa ya Samatta bado maisha ya TP Mazembe yalikuwa ndio njia yake kuu. Kuishi na kupendwa na Moise Katumbi Chapwe ilikuwa ni jambo bora na alipata mwanga wa kibiashara na namna ya kuishi kifalme.
Ndio, aliposhinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ndipo wengi tulipoamini kuwa kila kitu kinawezekana.
Leo hii tunazungumzia Mbwana Samatta aliyeona kuwa wakala wake alikuwa anamchelewesha kiasi cha kuamua kuachana naye na kuwa chini ya mawakala wapya wanaoitwa SPOCS ambao leo hii wamemshusha kwenye jiji la Birmingham ili atue AstonVilla.
Lakini kila nikitazama katika viganja vyangu sioni jina ninaloliona likienda na kasi ya Samatta. Hapo alipo Msuva na kwa umri wake kajitahidi Ulaya itakuwa hatua kubwa ambayo ni nyongeza. Lakini kwanini inaonekana kuwa ngumu kwanini inaonekana miujiza mpaka leo hii ambapo dunia ya teknolojia inaturuhusu kufikiana bila kushikana mikono?
Azam waliwahi kuwa na Chilunda na Farid Mussa na wangeweza kuwa na wengi zaidi. Yanga waliwahi kuwa na Shabani Nonda na wanajivunia mpaka leo. Kila nikitazama tabasamu la Samatta, natizama chini na kuona nembo ya klabu zetu hizi. Nembo zilizodumu kwa miaka ya babu wa babu yangu na nyingine zilizoanzishwa kwa fedha nyingi lakini bado vyote vinaishi dunia ya uongo, dunia ya kupiga ramli na kuomba chini ya mbuyu mema yatokee, wapate mwingine kama huyu bila kuweka mipango bali kwa kuomba miungu isiyokuwepo.
Simba leo hii, viongozi wake wanarukaruka kwa furaha kwa sababu italipwa kiasi cha usajili cha Samatta mpaka atakapostaafu, kila anapouzwa Simba watapata walau asilimia 0.5 mpaka 1 ya dau la usajili la Samatta. Wote wanapiga kelele kuhusu hela ya Aston Villa, Yanga wanatamani wangekuwa wameuza ili hela hizi za ziwafikie, Azam wanatazama saa hawawezi kurudisha nyakati nyuma wabadili sera zao za sasa.
Hizi ni hesabu nyepesi ambazo wenzetu huzifanya kila kukicha, hizi ni hesabu ambazo Genk wanatamani wangempata Samatta akiwa na miaka 17, hesabu ambazo Benfica wanaziishi kila siku. Kuwa na utaratibu ambao unazalisha au kununua wachezaji vijana wenye  vipaji haswa na unaweka utaratibu wa kuwasaidia kwenye usimamizi wa vipaji vyao. Sio tu kwamba vilabu hivi vitanufaika kwa kuwa na timu imara na yenye filosofia bora bali pia watakuwa wanajiweka kwenye mazingira ya kuuza na kuendelea kunufaika na wachezaji hawa kwa miaka yote ya maisha yao ya mpira.