Mbona iko hivi: Unisamehe Samatta, sikukuelewa

Muktasari:

Nakumbuka Samatta alitusikiliza vizuri lakini alikataa. Pembeni aliniambia kwamba yeye lengo lake ni kucheza katika mojawapo ya ligi kubwa za dunia ili afungue milango kwa Watanzania wenzake. Kama angekubali kwenda Qatar, angekuwa ameonyesha ubinafsi mkubwa.

JANA Ijumaa Watanzania wengi mashabiki na wasio mashabiki wa mchezo wa soka waliamka wakiwa na furaha baada ya kuhakikishiwa kwamba uhamisho wa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, kutoka Genk kwenda Aston Villa utafanikiwa.
Ni jambo la kihistoria kwa taifa letu. Mimi ni msomaji wa magazeti makubwa ya nje ya Tanzania na kulikuwa na kipindi juzi jioni ambako karibu vyombo vyote vikubwa vya habari vilikuwa na habari ya Samatta.
Hatuwezi, walau kwa sasa, kujua nini maana ya tukio hili. Hata hivyo, tunaweza tu kubashiri kwamba alichofanya Samatta kitafungua milango kwa wachezaji wa Kitanzania katika soka la kimataifa. Siku ambayo ataichezea Aston Villa kwa mara ya kwanza, jina la nchi yetu litaingia katika vitabu vya historia ya Ligi Kuu ya England.
Wiki iliyopita niliandika hapa kuhusu umahiri wa Emmanuel Okwi lakini ukweli mchungu ni kwamba hajawahi kucheza popote katika ligi ya kiwango cha Genk wala Aston Villa anakokwenda Samatta. Haitoshi tu kusema Okwi, sikumbuki kama taifa zima la Uganda limewahi kuwa na mchezaji katika Ligi Kuu ya Uganda.
Kuna mataifa kama Burundi yamewahi kuwa na wachezaji katika Ligi Kuu ya England kama kina Saido Berahino na Gael Bigirimana lakini ukichunguza kiundani utabaini walifaidika zaidi na kuzaliwa kwao na kukulia Ulaya na si kwa sababu ya viwango vyao.
Lakini Samatta ni mtoto wa Mbagala hapa Dar es Salaam. Miaka 20 iliyopita, wakati Samatta akiwa mdogo sana na mimi mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Forodhani hapa Dar es Salaam nakumbuka tulikuwa tukimcheka Abdallah Ulega – ambaye sasa ni Naibu Waziri katika Serikali ya Rais John Magufuli, kila alipojitambulisha kwamba yeye anaishi Mbagala.
Mbagala!!!!! Nani alitaka kukulia na kulelewa Mbagala wakati huo? Lakini ndiyo huko Mbwana alipoanzia kucheza soka na kuonyesha uwezo wake. Na ukizungumza naye atakwambia kulikuwa na watu wanaujua kuliko yeye isipokuwa tu yeye alikuwa na juhudi za ziada na hakuwa na mambo mengi.
Nimemtazama Mbwana kwa karibu miaka kumi hivi. Wakati naingia Simba kama msemaji wa klabu, yeye ndiye aliyekuwa amemaliza mgogoro wake na viongozi uliosababisha asuse kucheza kwa muda na akawa ameanza kucheza kwa kiwango cha juu sana.
Nilikuwa Uwanja Mkuu wa Taifa siku Simba chini ya Patrick Phiri ilipofungwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mechi ya kukumbukwa iliyomtangaza kijana huyu kwenye soka la kimataifa. Dakika zile 90 za kukumbukwa zilimfanya mmiliki wa Wakongo wale, Moise Katumbi, kukubali kufungua pochi lake na kumsajili Samatta.
Mbwana akawa nyota Mazembe. Ikafikia wakati akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa Afrika miongoni mwa wale waliokuwa wakicheza katika ligi za ndani ya Afrika. Likawa ni suala la muda tu kabla hajapata timu ya kuchezea Ulaya.
Siku chache kabla Mbwana hajaenda Genk, nilipata ugeni wa wakala wa kimataifa wa wachezaji na rafiki yangu, Mamadou Adrien Thiam. Yeye alikuwa amepata timu kutoka Qatar iliyokuwa ikimtaka Samatta kwa gharama yoyote. Zaidi ya fedha ya kumsajili kutoka Mazembe, walikuwa tayari kumpa mchezaji huyo kiasi cha dola za Marekani milioni moja (shilingi bilioni mbili) kama gharama za kumsajili.
Mamadou alitaka nisaidie kumbembeleza Samatta akubali ofa hiyo. Tulikwenda katika Hoteli ya Lamada, Ilala ambako Mbwana alikuwa akipenda kufikia kila aliporejea Tanzania kutoka Congo kwa sababu hakuwa akipata muda wa kutosha kupumzika akienda kwao Mbagala.
Nakumbuka Samatta alitusikiliza vizuri lakini alikataa. Pembeni aliniambia kwamba yeye lengo lake ni kucheza katika mojawapo ya ligi kubwa za dunia ili afungue milango kwa Watanzania wenzake. Kama angekubali kwenda Qatar, angekuwa ameonyesha ubinafsi mkubwa.
Sikumuelewa kwa sababu sikuelewa mtu anakataaje shilingi bilioni mbili ambazo zingetosha kununua nyumba katika eneo lolote alilotaka yeye la Dar es Salaam na kuanzisha mradi ambao ungempa fedha katika miaka yake baada ya kustaafu kucheza soka.
 Nakumbuka nilimwambia atakuja kujuta baadaye kwa uamuzi wake huo. Hata hivyo, sasa naamini alikuwa sahihi wakati ule kwa kukubali kukosa mabilioni ya shilingi kwa sababu tu ya kutaka kutimiza ndoto zake.
Wakati mwingine, kutimiza ndoto ni jambo la maana kuliko utajiri. Baada ya kwenda Mazembe, Samatta alifungua njia kwa kina Ramadhani Singano na sasa nafahamu Genk watakuwa na Kelvin John ‘Mbappe’ baada ya Mbwana.
Kwa sababu hii, nina uhakika kwamba mara baada ya Samatta kumaliza muda wake England, kutakuwa na Mtanzania mwingine katika ligi hiyo mashuhuri kwa sababu kila wakati Mbwana amekuwa na tabia ya kuacha alama anakokwenda.
Sikuwa sahihi wakati ule nikimshauri Mbwana akubali kwenda Uarabuni.
Ndiyo sababu ni muhimu kutumia fursa hii kumwomba radhi na kumtakia kila la kheri katika maisha yake mapya kwenye Ligi Kuu ya England.