Sababu sita za Aussems kung'oka Simba SC

Muktasari:

Aussems aliyetua Msimbazi Julai mwaka jana kuchukua nafasi ya Mfaransa Pierre Lechantre na kuiwezesha Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea taji la Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kutwaa Ngao ya Jamii mara mbili, amehitimisha maisha yake klabuni hapo.

Dar es Salaam. KUSHNEI! Klabu ya Simba imetangaza rasmi sasa kuachana na Kocha Mkuu wake, Patrick Aussems kuhitimisha kile ambacho Mwanaspoti kwa wiki kadhaa sasa imekuwa ikikiripoti, walishamaliza kila kitu isipokuwa ilisubiriwa siku ya kutangaza tu na jana wakafanya hivyo zikitajwa sababu sita.
Kocha Aussems naye alithibitisha kutimuliwa Simba mara baada ya mchana wa jana kufanya kikao na Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ikiwa ni saa chache tangu Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo kukutana na kocha huyo na kukabidhi maamuzi waliyoafikiana kwa mabosi wa Simba.
Aussems aliyetua Msimbazi Julai mwaka jana kuchukua nafasi ya Mfaransa Pierre Lechantre na kuiwezesha Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea taji la Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kutwaa Ngao ya Jamii mara mbili, amehitimisha maisha yake klabuni hapo.
Simba ilimtambulisha Aussems Julai 20, 2018 baada ya kusaini mkataba wa kuinoa klabu hiyo na kutangazwa kutimuliwa kazini jana Jumamosi imehitimisha siku 498 za kuwepo kwake Msimbazi, huku mambo manne yakitajwa kama sababu ya kufukuzwa akiiacha timu kileleni ikiwa na pointi 25.
Pande hizo mbili zimeachana baada ya vita ya kisheria, ikiwa ni siku chache tangu wamsimamishe kazi kwa muda ili kutaka atoe utetezi wa makosa yaliyokuwa yakimkabili na alienda kujitetea mbele ya Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Moses Kaluwa.
Kikao cha jana kati ya Senzo na Aussems kimehitimisha kile kilichokuwa kikielezwa na Mwanaspoti mapema tangu mwezi uliopita, kabla ya jana pande hizo kuthibitisha kuachana kwao, huku zikitajwa sababu sita za kutemwa kwa kocha huyo ambaye atafidiwa mshahara wa mwezi mmoja tu ambao ni Sh25 milioni sambamba na tiketi ya ndege ya kurejea kwao, huku Senzo akiachiwa msala sasa wa kusimamia mchakato wa kuleta kocha mkuu mpya, ili kudhibiti hila za upigaji wa fedha.

SABABU HIZI HAPA
Taarifa kutoka ndani ya Simba na zilizokuja kuthibitishwa baadaye jioni na klabu hiyo kupitia Senzo ni kitendo chake cha kujieleza juu ya safari yake ya siku mbili nje ya nchi bila kuaga ikielezwa alitimkia Afrika Kusini kumalizana na klabu moja ya Ligi Kuu nchini humo.
Aussems alitakiwa kuthibitisha hakwenda Afrika Kusini kama anavyosisitiza mwenyewe, akidai ilikuwa safari binafsi ya kwenda kutatua matatizo ya kifamilia.
Inaelezwa Aussems alibanwa aonyeshe tiketi kama kweli hakwenda Sauzi na yeye akigoma kutoa ushirikiano wa kutoa nyaraka za tiketi ya safari yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Senzo, inasema kilichomwondoa ni kushindwa kutekeleza malengo ya klabu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, 2019-2020 ya kutakiwa timu ifike makundi na badala yake kutolewa raundi ya awali na UD Songo ya Msumbiji.
Pia alishindwa kusimamia malengo ya klabu licha ya kutolewa Afrika kwa kutosimamia ari na nidhamu ya wachezaji kwa michuano ya ndani na nje.

SABABU NYINGINE
Licha ya taarifa ya Simba kuanika sababu hizo, lakini mmoja wa vigogo wa klabu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina alilidokeza Mwanaspoti; “Kuna makosa mengi aliyoshtakiwa nayo kwa kamati ya nidhamu, lakini ukweli jamaa alikuwa haambiliki na aliyekosana na Mtendaji wa zamani na hata wa sasa, sambamba na kiburi chake cha kukataa kukaa kambini na kung’ang’ania hotelini.”
Sababu nyingine iliyotajwa kuchangia kocha huyo kuondoka ni kukataa wachezaji kukaa kambini badala yake alikuwa akitaka wachezaji waende siku moja kabla ya mechi, ilihali kambi ikilipiwa mwaka mzima.
“Pia hajawahi kutoa ripoti yoyote ya kitaalamu ya msimu kama ambavyo aliagizwa kuhusu kazi yake na sababu nyingine ni kutokuwa na mawasiliano mazuri na viongozi wa juu, pia kukataa kwake kupewa nyumba badala yake tangu alipofika nchini amekuwa akikaa hotelini tu.
Taarifa zaidi zinasema, Aussems alitakiwa kukabidhi kila kitu ambacho hakikuwa ndani ya mkataba wao, ikiwamo kompyuta mpakato aliyokuwa akiitumia tangu atue Msimbazi kisha aangalie ustaarabu mwingine na alipotafutwa na Mwanaspoti jama mchana alithibitisha kila kitu.
Cheki mazungumzo hayo mafupi ya Mwanaspoti na Aussems kabla ya jioni yake kuanika kutimuliwa kwake na Simba kutuhibitisha kwa kutoa taarifa rasmi ya kuhitihimisha ndoa yao ya takribani mwaka mmoja na nusu;

Mwanaspoti: Patrick Aussems habari ya mchana kaka!
Aussems: Salama habari ya kwako rafiki
Mwanaspoti : Jumamosi yetu iko salama tunashukuru
Aussems: Niambie rafiki nimepokea simu yako kwa heshima tu
Mwanaspoti: Nashukuru Patrick, vipi kaka ulikutana na Mtendaji Mkuu wa Simba leo? Tulisikia kuna hicho kikao cha nyie wawili...!
Aussems: Ndio nilikutana naye, naona jambo limekamilika.
Mwanaspoti: Unamaanisha nini kusema jambo limekamilika?
Aussems: Klabu imenifukuza kazi rasmi, nafikiri nitafute baadaye kidogo tutaongea zaidi kuna mambo ya mawasiliano nayafanya.
Mwanaspoti: Pole sana Patrick, sababu ni ipi?
Aussems: Nimeambiwa matokeo mabaya
Mwanaspoti: Sababu ni hiyo kweli?
Aussems: Rafiki yangu naomba nitafute baadaye tutaongea zaidi kuna mawasiliano nayafanya na familia, tutaongea zaidi baadaye.
Mwanaspoti: Ok, sawa Patrick basi tutakutafuta hiyo baadaye.
Aussems: Ahsante sana, baadaye