Ronaldo, Mbappe uso kwa uso Euro 2020

Muktasari:

Katika Kundi F linalotajwa kama ‘kundi la kifo’, mbali na Ufaransa na Ureno, wapo pia miamba ya soka duniani, Ujerumani. Ureno na Ufaransa itakuwa marudio ya fainali ya Euro 2016.

London, England. Cristiano Ronaldo na chama lake la Ureno watakuwa na shughuli pevu ya kuwakabili mabingwa wa dunia, Ufaransa, wenye mastaa kibao kama Kylian Mbappe, Antoine Griezmann, N’Golo Kante na Paul Pogba, kwa mujibu wa droo ya makundi ya fainali za Mataifa ya Ulaya (Euro) 2020 iliyopangwa wikiendi.
Katika Kundi F linalotajwa kama ‘kundi la kifo’, mbali na Ufaransa na Ureno, wapo pia miamba ya soka duniani, Ujerumani. Ureno na Ufaransa itakuwa marudio ya fainali ya Euro 2016.
England imepangwa kundi moja na Croatia na Jamhuri ya Czech, huku supastaa Gareth Bale na chama lake la Wales akiwa na shughuli ya kuzikabili Italia, Uswisi na Uturuki kwenye Kundi A.
England na Croatia ya Luka Modric itakuwa marudio ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Wembley, Juni 14 mwakani.  Michuano hiyo itafunguliwa kwa mechi kati ya Italia na Uturuki itakayopigwa mjini Rome, Juni 12.
Katika mfumo mpya, fainali hizo zitafanyika kwenye miji 12 tofauti ya Ulaya, ikiwa ni kusherehekea miaka 60 tangu michuano hiyo ilipoanzishwa.
KundiA: Italia, Uswisi, Uturuki, Wales
Kundi B: Ubelgiji, Russia, Denmark, Finland. Kundi C: Ukraine, Uholanzi, Austria, mshindi wa mchujo D/A
Kundi D: England, Croatia, Czech, mshindi wa mchujo C
Kundi E: Hispania, Poland, Sweden, mshindi wa mchujo B
Kundi F: Ujerumani, Ufaransa, Ureno, mshindi wa mchujo A/D