PSG yaingia anga za Manchester City yamtaka PEP

Muktasari:

Guardiola mkataba wake huko Man City utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao, lakini kumekuwa na kelele nyingi kwamba maisha yake huko Etihad yanaweza kufiki mwisho msimu huu utakapotia nanga baada ya timu hiyo kushindwa kuwa na maajabu kwenye Ligi Kuu England ambapo mastaa wake wengi wakionekana kwamba pumzi zimeshaanza kukata

PARIS, UFARANSA. Manchester City wanapanga yao. Paris-Saint Germain nao wanapanga yao.
Ni kuhusu kocha Pep Guardiola. Mabosi wa Man City wanapambana kwa kadri wanavyoweza kuhakikisha Mhispaniola huyo anabaki Etihad akiendelea kuijenga timu yao.
Lakini, PSG wao wamechungulia na kuona Guardiola ndiye mtu anayewafaa kwenda kutimiza mambo yao yote wanayoyataka ambayo yamekwama. Dhamira ya PSG ni kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika kutimiza ndoto hizo wamefanya usajili wa nyota wote muhimu wakiwanasa kwenye kikosi chao, lakini shida wanadhani sasa imebaki kwenye kocha bora. Ndoto kama hizo za kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya zipo pia Man City, lakini mastaa wake ni tofauti na wale waliopo huko Paris.
Kwenye kikosi cha PSG kuna mastaa wote wenye uwezo wa kukupa taji la ubingwa huo wa Ulaya. Sasa mabosi wa mabingwa hao wa Ufaransa wameona jibu la swali lao hilo ni moja tu, kwenda kumchukua Guardiola wakati watakapoamua kumfungulia mlango wa kutokea Mjerumani Thomas Tuchel.
Guardiola mkataba wake huko Man City utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao, lakini kumekuwa na kelele nyingi kwamba maisha yake huko Etihad yanaweza kufiki mwisho msimu huu utakapotia nanga baada ya timu hiyo kushindwa kuwa na maajabu kwenye Ligi Kuu England ambapo mastaa wake wengi wakionekana kwamba pumzi zimeshaanza kukata.
Kitu kingine ni kwamba mkewe Guardiola ameshaondoka Manchester akirudi kwao Hispania jambo linaloelezwa kwamba huenda likamchochea pia kocha huyo kuamua kubadilisha upepo licha ya kudai kwamba hana mpango kuondoka hadi mkataba wake utakapofika mwisho. Baada ya kubeba mataji yote matatu England msimu uliopita, Man City msimu huu haonekani kuwa na maajabu kwenye Ligi Kuu England wakiachwa kwa zaidi ya pointi 13 na vinara Liverpool na mambo yalitibuka zaidi baada ya sare yao ya 2-2 Etihad dhidi ya Crystal Palace. Pengo hilo la pointi hapo Liverpool ilikuwa kabla hawajacheza na Manchester United jana Jumapili huku wakiwa na mchezo mmoja mwingine mkononi dhidi ya West Ham United.
Mkewe Guardiola, mrembo Cristina alirudi zake Barceona mwaka jana kwenda kuendelea na biashara zake za mitindo.
Kocha huyo, Guardiola ambaye amesema kwa asilimia 100 atabaki Etihad msimu ujao, bado anazua hofu kutokana na mkwanja mrefu wanaomiliki PSG  ambao wapo tayari kumwekea mezani kocha huyo kumchukua.
Taarifa zinabainisha kwamba mmiliki wa PSG anamini Guardiola ndiye kocha aliyebaki ambaye akija kwenye kikosi chao atawafanya kuwa tishio zaidi Ulaya nzima.
Lakini, vita itakuwa kubwa kwa sababu Man City mpango wao ni kumpa dili jipya Guardiola ili kukata watu maini wanaomfukuzia kocha wao. Guardiola alipoulizwa kuhusu hatima yake baada ya sare dhidi ya Palace, Mhispaniola huyo alisema: “Labda kama watanifukuza, nitabaki hapa kwa asilimia 100. Si kwamba kwa sababu tumeshinda mechi mbili zilizopita, hata kama mambo yangekuwa hovyo, nisingeondoka kwenda kikote.