Nyuma ya pazia: Kwa Ole vimebaki unafiki na aibu tu

Muktasari:

Mbaya zaidi Ole anachanganya bwana. Leo anafungwa na Sheffield United halafu wiki ijayo anatoka sare na Liverpool. Baadaye akafanya mambo ya ovyo. Akafungwa na timu ya kijinga kisha akawachapa Tottenham Hotspurs na Manchester City ndani ya siku nne.

OLE at the wheel’ alisikika Rio Ferdinand wakati dunia ikiwa imegeuka kuuingia mwaka jana. Alimaanisha ‘Ole yupo katika usukani’. Wakati huo Rio alikuwa anatabasamu usoni. Sehemu ya ndani ya moyo wake ilikuwa inasema ‘Huyu ndiye mwanaume’.
Wakati huo United wakianza kung’ara upya chini ya Ole Gunnar Solskjaer baada ya kufukuzwa kwa Jose Mourinho. Paul Pogba alionekana amezaliwa upya. United ikaanza kushambulia kama timu. Wachezaji wakacheza kama timu. Picha zikawaonyesha Paul Pogba na Ole Gunnar wakitabasamu. Kabla ya hapo picha mara nyingi zilikuwa zikiwaonyesha Mourinho na Pogba wakiwa wamenuniana.
Nyuma ya kauli ya Rio kulikuwa na wenzake wakijisemea hivyohivyo. ‘huyu ndiye mwanaume’. ‘huyu ndiye ambaye anaifahamu United nje ndani’. Mwingine angeweza kusema ‘United imerudi katika tamaduni zake’.
Rio alikuwa anawakilisha mioyo ya kina Roy Keane, Gary Neville, Paul Scholes, lakini zaidi. Baba yao. Sir Alex Ferguson. Wahifadhina hawa walikuwa wanajisemea ‘United imerudi katika mikono yao’. Wakati ule wa Mourinho kila kichapo cha United kilikuwa kinakwenda katika mikono yake.
Mourinho alikuwa anashambuliwa kila siku na kina Scholes katika meza za uchambuzi. Kiburi chake kilimsaidia kwa sababu alitaka kina Scholes wakae kando. Akawaambia wazi kwamba United kushika nafasi ya pili nyuma ya City yalikuwa mafanikio makubwa kwake. Akabezwa.  
Leo kina Rio wanatazamana kwa aibu. Kila kichapo wanakipeleka katika mikono ya wachezaji. Kisa? Wanamlinda Ole. Ole amevunja rekodi zote za ubovu pale Old Trafford, lakini wenzake wameishia kutuonyesha sura za fadhaa tu.
Mbaya zaidi Ole anachanganya bwana. Leo anafungwa na Sheffield United halafu wiki ijayo anatoka sare na Liverpool. Baadaye akafanya mambo ya ovyo. Akafungwa na timu ya kijinga kisha akawachapa Tottenham Hotspurs na Manchester City ndani ya siku nne.
Mpaka pale alikuwa anawachanganya United. Alikuwa anajua namna ya kuvuta muda. Wakati ukitazamia apoteze mechi, ndio kwanza alikuwa anashinda mechi muhimu. Lakini baada ya vichapo vya Arsenal na hiki cha juzi cha City, Ole anajiondolea sifa ya kuwa kocha wa mechi kubwa. Kwa sasa kina Rio wana sura za aibu zaidi. Rafiki yangu Roy Keane amekuwa kimya kwa sababu huwa anaitwa hata mazoezini na Ole kwa ajili ya kuongea na vijana.
Ukweli ulio wazi ni kwamba Ole si kocha wa kuifundisha United tena. Mbaya zaidi kuna mambo mawili. Kwanza wanaona aibu kumfukuza. Ole hawezi kuachia ngazi kwa sababu akiachia ngazi mwenyewe United hawatamlipa fidia.
Pili, wakati huu wakiona aibu kumfukuza Ole, kuna makocha wawili bora hawana timu. Mauricio Pochettino na Max Allegri. Roy Keane anajua hili. Rio Ferdinand anafahamu hili. Gary Neville anajua hili. Tatizo hawawezi kutamka Ole aondoke na Pochettino aingie kazini.
Ni mwenzao. Kwao utakuwa usaliti mkubwa. Kama anayefanya mambo haya angekuwa Mourinho basi ingekuwa rahisi tu kunyanyua mdomo na kumtaka Mourinho aondoke na nafasi yake ichukuliwe na Poche. Lakini huyu Ole ni mwenzao.
Na sasa tunaendelea kutazama movie hii inayoitwa ‘Subira’. Sijui itakwenda mpaka lini lakini ni wazi haina mwisho mrefu. Katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto mwaka juzi, Bosi Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward aligoma kumpa pesa za manunuzi ya wachezaji Mourinho akiamini hakuwa mtu sahihi wa kutumia pesa zao.
Wakati ule Mourinho alikuwa akimtaka Harry Maguire. Hawakuona kama alikuwa anaipeleka timu katika mwelekeo sahihi. Leo dirisha la Januari limefunguliwa na nataka kuona kama Woodward anaweza kumpa pesa Ole tena baada ya kumpatia pesa za Aaron Wan-Bissaka na Maguire lakini mambo bado mazito.
Ni nyakati kama hizi ambapo Woodward anajua ni bora umpatie pesa Pochettino anunue wachezaji na kuigeuza United kuwa kama Spurs ya miaka ya karibuni ilivyokuwa. Kina Neville wanajua hili lakini hawawezi kusema. Ole ni mwenzao.
Siioni United ikisogea mbali chini ya Ole. Yalikuwa ni makosa makubwa kwa United kumpatia Ole kibarua cha kudumu. Na sasa wanaona makosa waliyoyafanya na mbaya zaidi wamejizungusha katika kitanzi ambacho ni kigumu kwao kukivua kutoka shingoni.
Arsenal nao wangeweza kufanya kosa kama hilo kama Fredrick Ljungberg angepewa kibarua cha kudumu. Bahati yao ni kwamba ilitokea tu Ljungberg aligeuka kuwa mmoja kati ya makocha wabovu wa muda katika historia ya Ligi Kuu ya England.
Mwisho wa siku tunaendelea kusubiri kitakachotokea Old Trafford. Mpaka kwa sasa kilichobaki katika kumfukuza Ole ni mambo mawili tu. Aibu na unafiki. Kina Scholes na Keane wanajua kwamba hafai na hawezi kuwafikisha popote, lakini wanahofia kula maneno yao.
Haya yanatokea wakati kule London Kaskazini Arsenal wanaanza kuimarika. Hilo linatokea wakati Frank Lampard naye ameanza kuiimarisha Chelsea. United wasihofie kumtafuna jongoo kwa meno. Wanaweza kujikuta wakiangukia mbali zaidi kama hawatafanya maamuzi magumu kwa sasa.
Kama Pochettino atakwenda kwingine, labda Bayern Munich. Kama Allegri atakwenda kwingine labda Barcelona, basi hizi ni nyakati ambazo United watazijutia. Watajutia maamuzi yao kwanini hawakumfukuza Ole mapema na kuwapa makocha wenye hadhi kazi yake.
Utaniuliza kama Pochettino ana hadhi hiyo lakini nitakujibu kwamba Pochettino ameipeleka Spurs katika ubingwa wa Ulaya bila ya kununua mchezaji wa Pauni 85 milioni kama Maguire.
 Lakini pia tazama alivyoibakisha Spurs katika Top Four kwa miaka mingi bila ya matumizi makubwa ya pesa.
Ukiniuliza kama Allegri ana hadhi hiyo nitakwambia katazame rekodi zake za Juventus kama zinasema uongo.
Narudia, kinachombakisha Ole kwa sasa katika kiti chake ni aibu na unafiki. Hasa kwa wale waliokuwa wanaongoza mashambulizi dhidi ya Mourinho. Leo wanaona aibu na wanajitahidi kuficha sura zao.