Nyuma ya Pazia: Huu ni Uhuni wa kina Raiola na waandishi wa habari

Saturday January 18 2020

Mwanaspoti-Nyuma ya Pazia-Tanzania-Michezo blog-MICHEZO-Mwanasport-Raiola

 

By Edo Kumwembe

MTU mmoja sasa hivi tunavyozungumza yupo mahala akijaribu kuidanganya dunia. Labda yupo katika chumba chake cha hoteli Paris. Labda yupo kando ya bwawa la kuogelea nyumbani kwake London. Simu ipo mkononi.
Anachofanya ni kuidanganya dunia kwa kujaribu kumjengea mazingira mteja wake afanikiwe.
Ananyanyua simu ya kwanza anapiga kwa rafiki yake mwandishi wa gazeti la The Sun la Uingereza. Anakata anapiga simu nyingine kwa mwandishi rafiki yake wa gazeti la Marca la Hispania.
Unajua anachoongea? Anadai mchezaji wake anatakiwa na klabu fulani. Anajua sio ukweli lakini anataka kuikumbusha dunia mchezaji wake anatakiwa kila mahala. Anajenga mazingira.
Haya ndio maisha ya mawakala. Umechoshwa kusoma uvumi unaohusisha wachezaji lukuki kuhamia katika klabu yako? Sikiliza vyema.
Mawakala wa soka ni wahuni ndio maana unaweza kusikia klabu yako Manchester United au Arsenal, au Liverpool, au Chelsea imehusishwa na wachezaji 50 ndani ya dirisha moja. Ni suala la uhuni na udalali tu. Wanachofanya mawakala ni kuwa karibu na waandishi na kuwaingiza katika mpangilio wa malipo yao kwa ajili ya kuhakikisha wanapitisha habari za wateja wao kutakiwa kila mahala ili wateja wao waonekane kama ni watu wanaotakiwa sana.
Leo utasikia Christian Eriksen anatakiwa na Manchester United, kesho utasikia anatakiwa na Real Madrid, keshokutwa utasikia ‘PSG wameingia katika mbio’ baada ya hapo utaambiwa Inter Milan wanamhitaji kuliko kiasi.
Kila siku jina la Eriksen litakuwa kila mahala. Kama leo uliiona habari ya Eriksen kuhusishwa kwenda Manchester United, keshokutwa utasikia habari ya kiungo mwingine kuhusishwa kwenda United na baada ya siku chache utasikia habari ya Mesut Ozil kwenda United na siku mbili baadaye utasikia United wapo mbioni kutoa dau kwa sababu ya James Maddison wa Leicester City.
Siku moja baada ya habari ya Maddison itakuja habari ya Manchester United kumtaka Jack Grealish.
Unajiuliza, ndani ya wiki moja inawezekana vipi Manchester United kutaka kununua viungo nane wa ushambuliaji?
Huwa naishia kucheka kwa sababu najua uhuni unaoendelea.
Kwa mfano, angalia jinsi ambavyo Erling Haaland alivyohusishwa na klabu nyingi za Ulaya baada ya kutambaz na klabu yake ya Salzburg msimu huu.
Wakala wake, Mino Raiola alitengeneza habari ya kutakiwa kila mahala kwa Haaland.
Ilionekana Haaland anatakiwa na Manchester United, Bayern Munich, Real Madrid, Juventus, Barcelona, Arsenal, Chelsea, Man City na kila timu kubwa ya Ulaya ambayo unaifahamu. Hapa Raiola alikuwa katika ubora wake wa kumnadi Haaland.
Hata hivyo kali ya yote ilikuja wakati Salzburg ilipocheza na Liverpool pale Austria. Kuna gazeti liliandika klabu 40 za Ulaya zilikuwa zimetuma maskauti wao nchini Austria kwa ajili ya kumtazama Haaland.
Hapo ndio unajiuliza, klabu arobaini? Kweli jamani?.
Unajua tu kwamba Raiola yupo kazini. Kwa aina yale ya mahitaji, kama kweli Haaland angekuwa anatakiwa kiasi hicho kupitiliza basi asingeishia Borussia Dortmund ambayo mwanzoni haikutajwa kabisa katika klabu ambazo zilikuwa zinamtaka Haaland.
Huu ndio uhuni wa akina Raiola na wenzake. Watu wengine ambao wanafanya uhuni huu kwa maamuzi yao wenyewe ni waandishi wa habari. Wanajitungia tu habari kwa sababu ya kuwatia matumaini mashabiki wa soka.
Kisaikolojia mwanadamu anapenda kufarijiwa kwa habari nzuri na sio mbaya. Hasa yule ambaye ameanza kukata tamaa.
Kwa mfano, mwandishi anajua kuwa Arsenal wana matatizo na safu yao ya ulinzi. Mwandishi anajua mashabiki wamechoshwa na akina Shkodran Mustafi. Anachofanya ni kuhakikisha anatunga habari ya kutia matumaini kwa mashabiki.
Hapo ndipo unaposikia ‘Arsenal yaingia katika mbio za Harry Maguire’. Kesho yake unasikia ‘Arsenal yaingia katika mbio za Kalidou Koulibaly’.
Unajiuliza, hawa mabeki wote thamani zao zinatajwa kuanzia pauni 80 milioni, Arsenal wanawezaje kununua beki wa bei ghali kiasi hicho?.
Hata hivyo habari hii inawafariji mashabiki wa Arsenal. Waandishi wanajua.
Ni kama vile ambapo wanaweza kusoma akili za mashabiki wa Manchester United na kugundua mashabiki wa United wanataka sana kuona timu hiyo inanunua kiungo mshambuliaji.
Ni hapo ndipo utakapogundua kila mwandishi anapambana kuihusisha United na kiungo fulani mshambuliaji. Watalikazania eneo hilo kwa muda mrefu na United inaweza kuhusishwa hata na viungo washambuliaji 10. Wanajua kwamba habari hiyo inafariji.
Ukiona uvumi mwingi jaribu kutulia tu na kuelekeza nguvu zako katika wachezaji ulionao. Kama habari inakaribia kuwa kweli basi kwa haraka haraka iamini mitandao miwili mikubwa. BBC na Sky Sports.
Habari ya Mtanzania, Mbwana Samatta kutakiwa na Aston Villa ilipofika katika mitandao hiyo ndipo unagundua ni kweli anatakiwa hasa. Magazeti ya nje usiyaamini sana. Akina Raiola wanakuwa kazini. Habari inatungiwa katika bwawa la kuogelea huku kando akiwa na chupa ya mvinyo.

Advertisement