Nyota kikapu waanika sababu kuitosa timu ya Taifa

Muktasari:

Endapo watafanya vizuri, timu hiyo itajiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika 2021.

Dar es Salaam.Wakati Tanzania ikishuka uwanjani katika mchezo wa kwanza wa kikapu wa kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika leo saa 12 jioni dhidi ya Kenya, nyota 10 kati ya 17 wa timu hiyo wameondoshwa kikosini.

Msafara wa Tanzania uliondoka juzi alfajiri kuelekea Nairobi Kenya kwa basi ukiwa na wachezaji saba pekee, huku waliosalia wakieleza sababu za kutojiunga na timu hiyo wakiwamo nyota watano wa JKT na wachezaji wa kulipwa kutoka nje ya nchi.

Awali Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) liliita nyota 17 ambao waliweka kambi ya wazi kwenye uwanja wa ndani ya Taifa huku wachezaji 10 kati yao hawakuambatana na timu hiyo nchini Kenya.

Wakizungumzia sakata hilo, baadhi ya wachezaji akiwamo aliyekuwa nahodha wa timu ya Taifa, Baraka Athumani walisema, Shirikisho na benchi la ufundi hawakutaka wasafiri na timu.

Baraka amesema utaratibu wa safari ya timu ya taifa uliwabagua baadhi ya wachezaji.

"Sikupenda tulivyofanyiwa, bora wasingetuita kwenye timu," alisema Baraka ambaye anashikilia tuzo ya mfungaji bora wa mashindano ya Afrika kanda ya tano msimu huu.

Alidai kocha na TBF waliitisha safari hiyo kienyeji bila kufuata taratibu.

"Wachezaji wa JKT ni watumishi wa Serikali na kocha wa timu ya taifa (Alfred Ngalaliji) anafahamu taratibu ili tuweze kusafiri na timu ya taifa tunapaswa kuombewa ruhusa, lakini hakufuata taratibu hizo kwa kigezo kwamba tuko likizo," alisema Baraka.

Jimmy Brown anayecheza nchini Philippines alisema amejiondoa kutokana na maandalizi hafifu.

Jimmy ambaye alijifua na timu hiyo kwenye uwanja wa ndani hadi siku ya mwisho kabla ya safari alisema utaratibu ambao TBF inautumia katika uteuzi wa timu ya taifa na maandalizi ndivyo vimemuondoa kikosini.

Ingawa rais wa TBF, Phares Magesa amekanusha akisema changamoto binafsi zilikwamisha wachezaji hao kutoambatana na timu.

Magesa alikiri baadhi ya wachezaji kujiondoa kwenye timu kwa sababu binafsi, lakini wengine hawakuwa na nyaraka muhimu za kusafiria (pasipoti).

"Wachezaji wa JKT wao ni suala lingine, lakini hiyo sisi haituhusu kwani kocha wa timu ya Taifa ndiye kocha wa JKT hivyo anafahamu taratibu zote," alisema.

Walioachwa mbali na Baraka na Jimmy wengine ni Musa Chacha, Kaikai Lek, Sudi Ulanga, Enrico Augustino, Cornelius Peter, Amin Mkosa, Fadhili Chuma, Mwalimu Heri, Jackson Brown na Gwalugano John.

"Baadhi yao waliomba udhuru, wengine walikuwa na matatizo ya kifamilia na wengine walitoka kwenye timu kwa sababu binafsi, tuwaombee waliopo Kenya wafanye vizuri," alisema.

Alisema wachezaji waliosafiri ndiyo wana vigezo kwani ndiyo walikuwa tayari kusafiri na timu hiyo ya taifa.

Wachezaji hao ni Stephano Mshana, Erick John, Ally Mohamed, Cornelius Peter, Ladislaus Lusajo, Issaya Aswile na Haji Mbegu ambao watakata utepe na wenyeji Kenya kwenye uwanja wa Nyayo.