Namungo yawatupia virago wanne wapo Mkongo na Muivory Coast

Muktasari:

Waliowatema ni Sina Jerome raia wa Kongo, beki wa kati Toure Leopold wa Ivory Coast, Omary Mponda na Juma Ali Babjey ambao ni wazawa

KATIKA kuhakikisha wanamaliza msimu wao wa kwanza wa Ligi kuu Bara kwa kishindo, Namungo FC imetangaza kuwatema nyota wake nne katika dirisha dogo litakalofunguliwa wikiendi hii kwa kutoridhishwa na viwango vyao.
Namungo ni kati ya timu mbili zilizopanda daraja msimu huu kutok Daraja la Kwanza (FDL) sawia na Polisi Tanzania ambao hata hivyo ni kama wamerejea tu, kwani ilishawahi kushiriki ligi kipindi ikifahamika kama Polisi Morogoro.
Mwenyekiti wa Namungo, Hassan Zidadu aliwataja waliowatema ni Sina Jerome raia wa Kongo, beki wa kati Toure Leopold wa Ivory Coast, Omary Mponda na Juma Ali Babjey ambao ni wazawa.
“Kila mchezaji alipewa masharti wakati anajiunga na timu, ikiwamo kuhakikisha anapata namba ya uhakika pamoja na kucheza mara kwa mara lakini wachezaji hao wameoneka kukosa nafasi.
“Hakuna mchezaji anayetudai mpaka sasa kila mchezaji ameshapewa stahiki zake, hivyo tunaachana nao na kuwatakia kheri huko waendako na bila shaka imefungua milango kwa wachezaji wengine,” alisema Zidadu.
Aliongeza pamoja na kuachana na wachezaji hao, Kocha Hitimana Thiery ameomba kuongezewa kikosini nyota wanne wa kuziba nafasi ya waliotemwa.
Nyota wa timu hiyo wameingia kambini wiki iliyopita kujiandaa michezo ya Ligi Kuu sambamba na michuano ya Kombe la FA wakipangwa kuvaana na Green Warriors, siku ya Desemba 22, mchezo utaofanyika kwenye Uwanja wa Majaliwa.
Green Warriors, ndio walioing’oa na kuwavua ubingwa Simba kwenye mechi ya raundi za awali za michuano hiyo ya FA kwa mwaka 2017 na kusababisha Kocha Joseph Omog kutemeshwa kibarua baada ya Msimbazi kufungwa kwa penalti 4-3, kutokana na dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.