Musonye ashangaa wachua misuli timu za wanawake ni wanaume

Muktasari:

Fainali ya Mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa wanawake itachezwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini kuanzia saa 10jioni.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye ameshauri wanawake kupewa kipaumbele katika kusimamia soka lao badala ya kuwatumia wanaume.

Musonye alisema soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati limepiga hatua, ni muhimu sasa hata maofisa wakawa ni akina mama.

"Tunataka kuona tunakuwa na makocha wanawake kama ambavyo Uganda na baadhi ya timu wamefanya, lakini hadi madaktari na wachua misuli.

“Inashangaza kuona timu ni za wanawake, lakini wachua misuli ni wanaume hiki kitu hakinifurahishi, wanawake waanze kufanya wenyewe," alisema Musonye.

Musonye pia ametoa wito kwa vyama na mashirikisho ya soka kuhakikisha timu za taifa za wanawake zinatinga katika mashindano ya dunia.