Mbelgiji wa Yanga kutesti mitambo kwa Kagera Sugar

Muktasari:

Hii ni mechi ya kwanza kwa kocha Luc Eymael tangu alipokabidhiwa jukumu la kuinoa Yanga wiki iliyopita

Dar es Salaam. Kocha mpya wa Yanga, Luc Eymael ameweka wazi anataka kukiona kikosi chake kikicheza soka safi la kushambulia kuanzia katika mchezo wa kesho Jumatano wa Ligi Kuu Tanzania dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mbelgiji huyo ambaye amewahi kuifundisha AFC Leopards ya Kenya mwaka 2013, alisema  amewasoma wapinzani wake kupitia ripoti ambayo amepewa  ili kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi katika mchezo huo.

“Sijawahi kuwaona wakicheza, lakini nimepewa ripoti inayowahusu imekuwa muongozo kwetu katika upande wa maandalizi. Binafsi nataka tucheze mpira wa chini, huwa nachukizwa na soka lakubutua butua, nimeona timu inawachezaji wenye utulivu.

“Kwangu ni suala la muda tu, tayari tumeshakuwa na msingi wa namna yetu ya kucheza, kila mchezaji amekuwa akijitoa ili kuhakikisha anakuwa na nafasi katika kikosi changu jambo ambalo limenivutia sana,” alisema kocha huyo.

Katika mazoezi ambayo Yanga, wamekuwa wakifanya chini ya Eymael walionekana kufanyia kazi zaidi namna ya kushambulia huku wakitumia maeneo ya pembeni, viungo ndio waliokuwa wakipewa jukumu la kuanzisha mshambulizi.

Haruna Niyonzima ambaye alikuwa akicheza katika eneo la kiungo alionekana kumudu vilivyo namna ya kuchezesha timu katika mazoezi hayo.

Alionekana Mrwanda huyo, kuwa mwenye utulivu zaidi  huku pasi zake zikiwa za uhakika, zilielekea  maeneo ya pembeni ambako mawinga  na mabeki walitakiwa kupita kwa kasi na kwenda kutengeneza nafasi za mabao.

Naye kocha wa Kagera Sugar, Macky Maxime alisema, “Yanga ni timu kubwa hilo tunalitambua, lakini hesabu zetu ni kupigania pointi tatu, hatuna hofu ya kukabiliana nao.”