Mbelgiji Luc aisuka Yanga ya mabao

Tuesday January 14 2020

Mwanaspoti-Mbelgiji-Luc-Tanzania-aisuka-Yanga-Mwanasport-Michezo-Michezoblog- mabao

 

By ELIYA SOLOMON NA THOMAS NG’ITU

Dar es Salaam. KOCHA mpya wa Yanga, Luc Eymael ameanza kukisuka kikosi chake kwa kufundisha mbinu mbalimbali za kushambulia huku mashambulizi hayo yakianzishwa na viungo wachezeshaji
Eymael akiwa na kocha aliyemtangulia, Charles Mkwasa jana kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria jijini Dar es Salaam, aliwatumia mabeki wa pembeni kupeleka mashambulizi huku akiwataka kuwa na utulivu mkubwa.
Kocha huyo alionekana zaidi akitumia mfumo wa 3-5-2 na 4-4-2 kwa kuwaanzisha kati mabeki watatu au wanne, lakini mfumo wa 3-5-2 aliutumia zaidi.
Eymael alikuwa hataki kabisa wachezaji wake wabutue, bali wacheze mpira wa pasi na hata mabeki wake nao kuanzisha mpira wa chini.
Hali hiyo ilifanya mazoezi yanayoendelea uwanjani hapo kuwa ya kuvutia kwani wachezaji walikuwa wakifuata wanachoelekezwa na kama wakikosea kocha wao alikuwa anawataka warudie.

HALI ILIVYOKUWA AWALI
Baada ya wachezaji kufika mazoezini kocha Eymael akiwa na benchi lake la ufundi, alitumia dakika nane kufanya mzungumzo na kikosi chake ambayo yalionekana kulenga kile ambacho alikuwa amekiandaa katika programu yake ya mazoezi.
Alionekana kuwa mtu asiyependa kupoteza muda kwani mara moja aliwataka wachezaji waanze mazoezi ya viungo ambayo yalifanywa kwa dakika 15, huku yakisimamiwa na kocha wa viungo Riedoh Berdien.
Mazoezi hayo yalifanywa na wachezaji wote kasoro makipa Metacha Mnata, Ramadhan Kabwili na Farouk Shikhalo ambao waliendelea na mazoezi  binafsi wakiwa na kocha wa makipa, Peter Manyika.
Wakati makipa wakiendelea na aina tofauti ya mazoezi huku dakika 15 za mazoezi ya viungo zikiwa zimemalizika, ndipo Berdien alipoamua kugawa makundi mawili ya wachezaji na kuanza mazoezi ya mbinu.
Katika makundi hayo lile la kwanza lilikuwa likisimamiwa na kocha mkuu, Eymael huku la pili likiwa chini ya kocha wa viungo ambaye alikuwa akisaidiana na Mkwasa.
Katika kila kundi ziligawanywa timu mbili ambazo zilikuwa zikicheza katika uzio maalumu huku ikisisitizwa kila mchezaji kuachia mpira kwa haraka kila alipokuwa nao, ambapo walikuwa wakijengewa uwezo wa kufanya uamuzi wa haraka.
Aina hiyo ya mazoezi ilitumia dakika 20, ambapo wachezaji walipata mapumziko ya kunywa maji na kisha kuungana na kuwa kundi moja kisha wote kuwa chini ya Eymael.

MABOSI MAZOEZINI
Wakati mazoezi hayo yakiendelea pembeni kulikuwa na wajumbe wa kamati wa Yanga wakiongozwa na Hersi Said, Arafat Haji na Salim Rupia.
Wakati mazoezi yanaanza Hersi alionekana kuzungumza mawili matatu na kocha huyo kisha wakaachana na kuendelea na mazoezi.
Mabosi hao walikuwa wakifuatilia mazoezi kwa umakini mkubwa muda wote mpaka walipomaliza na kuondoka.

DANTE AFUNGUKA
Beki wa kati wa klabu ya Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’ alisema kwamba kocha huyo amekuwa akiwasisitiza muda wote wacheze mpira wa chini na siyo kubutua.
“Kocha kama ambavyo mmemuona hapendi tubutue, si mabeki wala mchezaji yeyote yule, yeye anataka mpira uchezwe chini,” alisema.
Aliongeza kuwa katika upande wa ushambuliaji anataka washambulie kwa spidi.

Advertisement