Maguire ataka Manchester United irudi Top Four

Muktasari:

Man United hawajapoteza mechi kwenye Ligi Kuu England kwa mechi tano mfululizo huku wakipata ushindi kwenye mechi mbili mfululizo ikiwa ni mara yao ya kwanza tangu walipofanya hivyo mwezi Machi.

MANCHESTER, ENGLAND.BEKI ghali duniani, Harry Maguire ataamini washambuliaji wenye njaa wa Manchester United watapiga mzigo wa maana kuwasaidia kumaliza msimu ndani ya Top Four kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Ushindi wa Man United dhidi ya mahasimu wao Manchester City uliwapandisha hadi kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, pointi tano nyuma ya timu iliyopo kwenye nanfasi ya nne, ambayo ndiyo inayotoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Beki Maguire, ambaye alikuwa nahodha wa Man United kwenye ushindi huo wa Jumamosi, alisema: “Top Four sasa tumeanza kuiona, lakini yatupaswa kuendelea kupambana kupata matokeo haya. Kuanzia mwezi uliopita au zaidi, nikiwa beki nimekuwa nikiwaangalia washambuliaji na kuamini watatupigia tu mabao ya ushindi.
“Wale watu wetu wanne kwenye kipindi cha kwanza walikuwa na njaa. Walikuwa tishio kubwa kwa wapinzani, hakika walionyesha ukomavu kwa wapinzani. Naamini sasa wameanzna kuelewana. Lakini, tusibweteke na kujihasau, ule ulikuwa mshindi mkubwa na pointi tatu muhimu, tunapaswa kuendelea kufunga mabao.”
Man United hawajapoteza mechi kwenye Ligi Kuu England kwa mechi tano mfululizo huku wakipata ushindi kwenye mechi mbili mfululizo ikiwa ni mara yao ya kwanza tangu walipofanya hivyo mwezi Machi.
Maguire, 26, aliongeza: “Tunaona kabisa mwaka huu kwenye baadhi ya mechi hatukupata matokeo ambayo yalistahili kunyakua pointi tatu. Lakini, kwa mechi mbili zilizopita, sidhani kama kuna mwenye kutia shaka kuhusu matokeo ya ushindi tuliyopata, tulistahili.”