Mabeki wote Manchester United pancha

Muktasari:

Beki ghali, Harry Maguire yupo tayari kucheza akiwa na maumivu ili aitumikie timu kwenye mchezo wao dhidi ya Norwich City, yenye mshambuliaji hatari Teemu Pukki kuweka mambo sawa katika Ligi Kuu England.

MANCHESTER, ENGLAND. PHIL Jones na Victor Lindelof walipopangwa wenyewe Jumanne iliyopita kilichowakuta ni aibu. Hawakuweza kabisa kuendana na kasi ya washambuliaji wa Manchester City, ambapo hadi kufikia mapumziko tayari walikuwa wameokota mara tatu mipira kwenye nyavu zao, licha ya kwamba bao moja lilikuwa la kujifunga, Andreas Perreira.
Hakukuwa na namna, Perreira ilikuwa lazima arudi kusaidia kukaba kwa sababu mabeki waliopangwa hawakuwa na tofauti na chujio. Hata hivyo, Ole Gunnar Solskjaer hakuwa na jinsi, mabeki wake wengine wote wenye afadhali ni wagonjwa.
Beki ghali, Harry Maguire yupo tayari kucheza akiwa na maumivu ili aitumikie timu kwenye mchezo wao dhidi ya Norwich City, yenye mshambuliaji hatari Teemu Pukki kuweka mambo sawa katika Ligi Kuu England. Beki Maguire aliyenaswa kwa Pauni 85 milioni kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi mwaka jana, alipata maumivu ya nyonga kwenye mechi ya sare ya bila kufunga kwenye Kombe la FA dhidi ya Wolves na madaktari walikuwa na hofu huenda angekuwa nje kwa mwezi mmoja. Hakucheza dhidi ya Man City kwenye Kombe la Ligi wenzake walipochapwa 3-1.
Solskjaer sasa ana kibarua kimoja kinachomkabili, ni suala la kuamua tu kucheza kamari kwa kumtumia mchezaji huyo, kwa sababu kwa kufanya hivyo kunaweza kuongeza ukubwa wa tatizo na kulazimika kufanyiwa upasuaji. Man United ina mabeki wa kati wawili tu kwa sasa ambao ndio wapo fiti, wote ni majanga, vidumu vya petroli vijana wanasema, kwamba hawakawii kujiripua.
Ukimweka kando Maguire anayesumbuliwa na maumivu ya nyonga, mabeki wengine wagonjwa kwenye kikosi hicho cha Man United ni Marcos Rojo anayesumbuliwa na maumivu ya misuli, Eric Bailly anasumbuliwa na maumivu ya goti, Luke Shaw nni mgonjwa, Axel Tuanzebe ana maumivu ya poaja na Timothy Fosu-Mensah anasumbuliwa na maumivu ya goti. Hivyo ni rahisi tu kusema kwamba beki yote ya Man United ipo kwenye wodi ya wagonjwa, mbona kazi wanayo!
Msimu huu kwenye Ligi Kuu England, beki huyo ya Man United imeruhusu mabao 25, wakiizidi timu moja tu kati tano zilizopo juu kwenye msimamo, ambao ni Chelsea waliofungwa 29. Beki ya Liverpool ndio iliyofungwa mara chache zaidi kwenye orodha hiyo, mabao 14, wakifuatiwa na Leicester City mabao 19 na Manchester City imefungwa 24.