Liverpool yasaka kuvunja rekodi hizi msimu huu

Muktasari:

Kikosi hicho cha Jurgen Klopp kipo kileleni kwa sasa kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya Leicester City inayoshika nafasi ya pili, huku wakali hao wa Anfield wakiwa na mchezo mmoja mkononi, wakipambana kubeba ubingwa wao wa kwanza wa ligi tangu mwaka 1990.

LIVERPOOL, ENGLAND. LIVERPOOL mwaka wao huu. Wapo kwenye ubora mkubwa wa soka lao wakifukuzia kumaliza ukame wa kubeba taji la Ligi Kuu England walilolisubiri kwa miaka 30 sasa.
Kwenye Ligi Kuu England msimu huu wameshacheza mechi 20, wameshinda 19 na kutoka sare moja tu, huku pointi hizo mbili walizopoteza ilikuwa ugenini dhidi ya Manchester United, Oktoba mwaka jana.
Kikosi hicho cha Jurgen Klopp kipo kileleni kwa sasa kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya Leicester City inayoshika nafasi ya pili, huku wakali hao wa Anfield wakiwa na mchezo mmoja mkononi, wakipambana kubeba ubingwa wao wa kwanza wa ligi tangu mwaka 1990.
Hizi hapa rekodi 10 matata kabisa ambazo Liverpool inazifukuzia ndani ya mwaka huu ili kufanya msimu wao kuwa wa kukumbukwa kwenye mchakamchaka wao wa kulinyakua taji la Ligi Kuu England.

Mwanzo bora baada ya mechi 21
Baada ya kushinda kwenye mechi 19 na kutoka sare moja, Liverpool hadi sasa wameshavuna pointi 58. Mechi yao ijayo watakwenda kuifuata Tottenham Hotspur kesho Jumamosi na kama watashinda basi wataweka rekodi safi, wakiwapiku Manchester City, kasi yao ya msimu wa 2017/18, ambapo walivuna pointi 59 katika mechi 21. Liverpool wakishinda mechi hiyo ya 21 kwao, watafikisha pointi 61. Kila kitu kinaonekana kwenda vizuri kabisa wa wakali hao wa Anfield ambapo kila mchezaji akili yake ipo kwenye kuisaidia timu kushinda mechi zake.

Kushinda mara nyingi mfululizo nyumbani
Manchester City waliibuka na ushindi mara 20 mfululizo kwenye mechi zake za ligi ilizocheza uwanjani kwao, Etihad kati ya 2011 na 2012. Liverpool kwa sasa imeshinda mechi 18 mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Anfield, hivyo wamebakiza mechi mbili tu kufikia rekodi ya Manchester United, Southampton na West Ham United, ambazo zilikuwa moto kwa kushinda nyumbani mfululizo kwenye ligi. Liverpool wamebaki kuwa wababe pekee ndani ya msimu huu ambapo hadi sasa kwenye ligi bado hajawapoteza  mechi uwanjani Anfield.

Kushinda mara nyingi mfululizo
Liverpool walishinda mechi 17 mfululizo kuanzia Machi hadi Oktoba 2019 kabla ya kwenda kupata sare dhidi ya Manchester United uwanjani Old Trafford. Tangu wakati huo, imekuwa ikitoa tu dozi kwenye ligi, wakiwa wameshinda mechi 11 hadi sasa, wakiwa nyuma kwa mechi saba tu kuifikia rekodi ya Manchester City ya kushinda mechi 18 mfululizo kati ya Agosti na Desemba 2017. Liverpool watahitaji kushinda zote kuanzia sasa hadi Februari 29 watakapocheza dhidi ya Watford ili kuifikia rekodi hiyo matata.

Vichapo vichache ndani ya msimu
Timu pekee kwenye Ligi Kuu England ambayo ilicheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mechi walikuwa Arsenal msimu wa 2003/04, ambapo hawakuonja uchungu wowote wa kupoteza mechi na kupachika jina la Invincibles. Msimu uliopita, Liverpool wao walipoteza mechi moja tu na msimu huu wanataka kumaliza kwa ubora zaidi ikiwezekana wasipoteze mchezo wowote ili kutimiza rekodi yao ya kupoteza mechi chache au kutopoteza kabisa kwenye mchakamchaka huo wa Ligi Kuu England. Wameshacheza mechi 20 hawajafungwa.

Mechi nyingi bila ya kupoteza
Arsenal ile iliyokuwa moto chini ya kocha Mfaransa Arsene Wenger ilicheza mechi 49 bila ya kupoteza, ikiwamo za msimu wao wote wa 2003/04. Kikosi cha kocha Klopp, Liverpool kwa sasa chenyewe kimecheza mechi 37 bila ya kupoteza, wakiwa nyuma kwa mechi 12 kufikia rekodi hiyo ya Arsenal. Kuifikia rekodi hiyo, Liverpool watahitaji kukwepa kipigo kwenye mchezo dhidi ya mabingwa watetezi, Manchester City ili kuikaribia rekodi hiyo, ambayo wataifikia kwenye mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Aston Villa wiki itakayofuata.

Muda mrefu bila kupoteza
Kitu ambacho hakishangazi ni kwamba timu ile iliyocheza mechi nyingi bila ya kupoteza, bila shaka ndiyo iliyotumia muda mrefu ndani ya uwanja bila ya kupoteza mchezo. Arsenal ilitumia siku 537 bila ya kupoteza. Ushindi wao dhidi ya Sheffield United walioupata Januari 2 mwaka huu, uliwafanya Liverpool kucheza kwa mwaka mzima bila ya kupoteza kwenye ligi. Wakiendelea kukomaa hadi mwisho wa msimu, watavuka rekodi ya Arsenal, itakapofika mwisho wa Juni, kipindi cha msimu utakapokuwa umemalizika.

Kushinda mechi nyingi kwa msimu
Hii ni rekodi nyingine kwenye Ligi Kuu England, inashikiliwa na kikosi cha Pep Guardiola cha Manchester City. Katika misimu yote miwili iliyopita, kikosi hicho kimeshinda mechi 32 kati ya 38 kwa msimu na kubeba ubingwa. Liverpool kufikia rekodi hiyo msimu huu wanahitaji kushinda mechi 14 tu baada ya sasa kuwa wameshinda mechi 18. Liverpool wakifanikiwa kufikia rekodi hiyo ya kushinda mechi 32 bila ya shaka watakuwa hawana kitakachowafanya washindwe kubeba ubingwa wa ligi hiyo yenye ushindani mkali huko Ulaya.

Kushinda mechi nyingi za nyumbani kwa msimu
Haijawahi kutokea huko nyuma, timu kushinnda mechi zake zote za nyumbani ndani ya msimu mmoja. Chelsea 2005/06, Manchester United 2010/11 na Manchester City 011/12 na 2018/19, ambao walishinda mechi 18 za nyumbani.  Liverpool hadi sasa imeshashinda mechi 11 kwenye mechi za nyumbani, wanahitaji kushinda mara 19 kwenye mechi za nyumbani, kwa kuzichapa Manchester United, Southampton, West Ham, Bournemouth, Crystal Palace, Aston Villa, Burnley na Chelsea kufikia rekodi hiyo.
Kushinda mechi nyingi za ugenini kwa msimu
Si kitu kinachoshangaza kuona timu inayoshika rekodi ya kushinda mechi nyingi za ugenini ndani ya msimu mmoja. Manchester City ndio wanaoshikilia rekodi hiyo baada ya kushinda mara 16 katika mechi 19 za ugenini walizocheza kwenye msimu wa 2017/18. Liverpool wameshinda mechi nane kati ya tisa za ugenini hadi sasa, kama wataibuka na ushindi mwingine basi utawahitaji kushinda mechi tisa kati ya 10 zilizobaki za ugenini kuweka rekodi hiyo matata. Hiyo ina maana kwamba watahitaji kushinda dhidi ya Tottenham, Wolves, West Ham, Norwich, Watford, Everton, Manchester City, Brighton, Arsenal na Newcastle.

Kuvuna pointi nyingi kwa msimu
Liverpool inashika namba tatu kwa kuwahi kuvuna pointi nyingi kwenye Ligi Kuu England, wakati msimu uliopita walipovuna 97.  Kwa bahati mbaya, hazikutosha kuwapa ubingwa, kwani Manchester City wao walimaliza wakiwa na pointi 98, hivyo wakawapiga kikumbo kwenye mbio za ubingwa. Man City pia waliweka rekodi ya kumaliza msimu wakiwa na pointi 100.  Kama Liverpool watashinda mechi zake zote zilizobaki ndani ya msimu huu, watavunja rekodi hizo na kwamba watamaliza msimu wakiwa na pointi 112, ambazo bila ya shaka zitaweka rekodi mpya kwenye Ligi Kuu England. Hapo bado wanaweza kutoka sare moja na kupoteza mechi tatu bado watakuwa na uwezo wa kuvunja rekodi hiyo ya Man City.