Lewandowski na wakali wa mabao manne UEFA

Muktasari:

Mbali na Lewandowski, wafuatao ni nyota ambao waliwahi kufunga mabao manne katika mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati yao ni pamoja na Lionel Messi wa FC Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Juventus.

Dakika 14 na sekunde 31 zilitosha kwa mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyepachika mabao manne ndani ya muda mfupi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mpoland huyo, aliweka rekodi hiyo usiku wa Jumanne ya wiki iliyopita wakati akiiongoza Bayern Munich ikijihakikishia kufuzu katika hatua ya mtoano baada ya kuifunga FK Crvena Zvezda ya Serbia kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Rajko Mitic mabao 6-0.

Lewandowski mwenye miaka 31, aliyafunga mabao yake katika mchezo huo katika dakika ya 53, 60, 64 na 68 huku mabao mengine ya Bayern Munich, yakifungwa na Leon Goretzka na Corentin Tolisso.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa Lewandowski kufunga mabao manne katika mchezo mmoja, mara yake ya kwanza ilikuwa kipindi alipokuwa akiichezea Borussia Dortmund, Aprili 24, 2013, alipoitungua Real Madrid mara nne katika ushindi wa 4-1.
Mbali na Lewandowski, wafuatao ni nyota ambao waliwahi kufunga mabao manne katika mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati yao ni pamoja na Lionel Messi wa FC Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Juventus.
Serge Gnabry
Nyota huyo wa zamani wa Arsenal, alifunga mabao manne katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Oktoba 22 dhidi ya Tottenham Hotspur ambao Bayern Munich waliibuka na ushindi wa mabao 7-2.Alitumia dakika ya 53, 55, 83 na 88 kufunga mabao hayo.
Katika mchezo huo, Lewandowski ambaye amekuwa akitegemewa na Bayern Kucheza kama mshambuliaji wa mwisho, alifunga mabao mawili.

Cristiano Ronaldo
Desemba 8, 2015, Ronaldo alifunga mabao manne kipindi hicho akiichezea Real Madrid katika mchezo ambao miamba hiyo ya soka la Hispania, waliitwanga Malmö FF ya Sweden mabao 8-0.
Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Ureno, alifunga mabao hayo dakika ya 39, 47, 50 na 58, Karim Benzema katika mchezo huo, alifunga mabao matatu ‘hat trick’.

Zlatan Ibrahimovic
Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita alifanya vizuri akiwa na LA Galaxy ya Marekani, alufunga mabao manne, Oktoba 23, 2013 wakati akiongoza Paris Saint-Germain ya Ufaransa kuizamisha Anderlecht ya Ubelgiji mabao 5–0. Alitumia dakika ya 17,22, 36 na 62 kufunga mabao hayo huku Edison Cavan akifunga moja.

Mario Gomez
Nyota huyo wa VfB Stuttgart, alifunga mabao manne, Machi 13, 2012 wakati ambao Bayern Munich ambayo alikuwa akiichezea ikiifunga mabao 7-0, Basel. Aliyafunga katika dakika ya 44,50, 61 na 67.

Bafetimbi Gomis
Gomis ambaye kwa sasa anaichezea Al-Hilal ya Saudi Arabia, alifunga mabao manne, Desemba 7, 2011 wakati iliyokuwa timu yake akiichezea Lyon ikiibuka na ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Dinamo Zagreb.

Lionel Messi
Messi ambaye anatajwa kuwa mmoja kati ya wanasoka bora duniani kwa sasa, alifunga mabao manne, Aprili 6, 2010 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa ambao FC Barcelona waliifunga Arsenal mabao 4-1.
Andriy Shevchenko
Novemba 25, 2005 akiwa katika kiwango bora na AC Milan ya Ligi Kuu Italia, Shevchenko ambaye pia aliwahi kuichezea Chelsea, alifunga mabao manne katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Fenerbahçe.

Ruud van Nistelrooy
Alifunga mabao manne akiwa na Manchester United, Novemba 3, 2004 katika mchezo ambao mashetani hao wekundu wa Old Trafford waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Sparta Prague.

Dado Prso
Alimaliza soka lake akiwa na Rangers ya Scotland, 2007, Prso , alifanya hivyo akiwa na Monaco na ilikuwa katika mchezo dhidi ya Deportivo La Coruña ya Hispania, timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 8-3, Novemba 5, 2003.

Simone Inzaghi
Machi 14, 2000 nyota huyo akiwa na Lazio, alifunga mabao manne katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Marseille, waliifunga mabao 5-1.

Marco van Basten
Ni mchezaji wa kwanza katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufunga mabao manne katika mchezo mmoja wa mashindano hayo, alifanya hivyo Novemba 25, 1992 akiwa na AC Milan, ilikuwa katika mchezo dhidi ya IFK Göteborg ambao walishinda kwa mabao 4-0.