Kiungo Akumu asajili Kaizer Chiefs

Muktasari:

Taarifa hizi zinakuja muda mfupi baada ya Chiefs, kutangaza kumuachia nyota wa zamani wa Simba SC, James Kotei

Nairobi. Kiungo wa kimataifa wa Kenya, Anthony Agay Akumu amekamilisha uhamisho wa kujiunga na miamba ya soka nchini Afrika Kusini, Kaizer Chiefs kwa kipindi kisichojulikana akitokea Zesco United ya Zambia.

Akumu ambaye ni mmoja wa mastaa watatu wa Kenya waliokuwa katika kikosi cha mabingwa hao wa Zambia, akiwemo Straika hatari Jesse Were na David Owino, ameondoka Zesco baada ya kumalizika kwa mkataba wake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaizer Chiefs, kupitia kwenye akaunti zao za mitandao ya jamii, haikuwekwa wazi kuwa, atakuwa klabuni hapo kwa muda gani, lakini ripoti zilizotufikia zinasema kuwa, huenda nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia, amesaini miaka mitatu na klabu hiyo.

Jina la Akumu, mwenye umri wa miaka 27, sio jina geni katika masikio na macho ya mashabiki wa Chiefs, kwani aliwahi kuwasababishia maumivu moyoni, alipowafunga katika michuano ya kombe la Shirikisho, bao lake likiwatupa nje ya michuano hiyo dhidi ya Zesco.

Akumu, ameichezea timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, mara 38 lakini pia amewahi kuichezea klabu ya Al-Khartoum ya Sudan aliyojiunga nayo, mwaka 2015, akitokea Gor Mahia.

Taarifa hizi zinakuja muda mfupi baada ya Chiefs, kutangaza kumuachia nyota wa zamani wa Simba SC, James Kotei pamoja na mchezaji mwenzake, Lorenzo Gordinho. Kotei anadaiwa kuwa njiani kujiunga na klabu ya Yanga SC.