VIDEO: Kilichombeba Mwakinyo kwa Tinampay hiki hapa

Muktasari:

Tinampay alicheza raundi zote bila kurudi nyuma huku Mwakinyo naye akitaka kucheza kwa kushindana naye mbinu ambayo ilikuwa ngumu kwa Mwakinyo kwani mpinzani wake alikuwa na nguvu.

USHINDI wa pointi aliopata bondia Hassan Mwakinyo dhidi ya Mfilipino, Arnel Tinampay, umekuwa gumzo mtaani, mashabiki wengine wakitofautiana wakiamini Mtanzania huyo ni kama amebebwa.
Wakati ushindi wa Mwakinyo dhidi ya  Tinampay wa Ufilipino ukiwa gumzo, mabondia wakongwe nchini wameeleza sababu zilizompa ushindi Mtanzania huyo.
Mwakinyo alitangazwa mshindi kwa pointi za majaji 2-1 kwenye Uwanja wa Uhuru juzi usiku katika pambano lililoteka hisia za mashabiki wa ndondi nchini huku Mwakinyo akikiri kushinda kwa tabu.

Alichokosea Mwakinyo
Katika pambano hilo, Tinampay alionekana kucheza kwa kujiamini zaidi na kutumia mbinu ya kutompa nafasi Mwakinyo  ambaye muda mwingi alikubali kubananishwa kwenye kona.
Tinampay alicheza raundi zote bila kurudi nyuma huku Mwakinyo naye akitaka kucheza kwa kushindana naye mbinu ambayo ilikuwa ngumu kwa Mwakinyo kwani mpinzani wake alikuwa na nguvu.
Ilimchukua muda mrefu Mwakinyo kumsoma mpinzani wake na kuanza kucheza kwa kupiga ngumi na kumkimbia, mbinu ambayo kama angeitumia tangu mapema ingempa tabu Mfilipino huyo.

Ubora wa Tinampay ulikuwa hivi
Ukiachana na uzoefu wa Tinampay ambao ni mara tatu ya Mwakinyo ulingoni, bondia huyo kutoka kambi ya Manny Pacquiao alikuwa akijiamini kupitiliza ulingoni na mara kadhaa  alionekana kutumia mbinu ya kumtisha Mwakinyo pale alipomkosakosa kwa makonde.
Raundi ya pili bondia huyo alifanya tukio lililoibua mjadala baada ya kuganda wima kwa sekunde kadhaa bila kufanya chochote zaidi ya kumkazia macho Mwakinyo katikati ya pambano na Mwakinyo kujikuta akishindwa kutumia nafasi hiyo kufanya chochote, tukio ambalo alilifanya pia raundi ya saba.

Glovu zatibua ratiba
Katika hali ya kushanga pambano hilo lilichelewa kwa kuanza kwa dakika kama 10 baada ya glovu za mabondia hao kutibua.
Ilianza kwa Tinampay ambaye alipanda ulingoni akiwa na glovu zake nyeupe, lakini akazuiliwa kuzitumia akitaka atumie za kamisheni wakihofu huenda kina kitu ameweka ndani,
ingawa ilikuwa tofauti alipovuliwa na kupewa nyingine ambazo hata hivyo zilikuwa kubwa na kulazimika kuzikaza kwa kuzungushia bandeji.
Baada ya Tinampay tatizo likawa kwa Mwakinyo ambaye glovu zake zilionekana kumbana na kulazimika kusubiri atafutiwe nyingine.

Kilichompa Mwakinyo ushindi hiki hapa?
Licha ya mashabiki kutoka uwanjani wakiwa wamegawanyika kwa matokeo ya Mwakinyo, mabondia wakongwe wamemaliza utata wakifafanua kilichombeba Mtanzania huyo juzi.
“Hata ningekuwa mimi jaji, Mfilipino ningempa ushindi katika raundi tatu pekee na raundi saba ningempa Mwakinyo,” alisema bondia wa zamani, Emmanuel Mlundwa ambaye alikuwa refarii wa pambano hilo.
Alisema katika ngumi, matokeo ya kila raundi yanajitegemea, bila kujali umepigwaje katika kila raundi.
“Anayeshinda anapewa pointi 10 na anayepigwa  anapewa pointi tisa, kama ukipigwa hadi kuhesabiwa ndipo unakatwa pointi moja na kupewa nane na aliyeshinda raundi hiyo anabaki na pointi zake 10.
“Katika lile pambano hakuna aliyehesabiwa na Mwakinyo alipiga ngumi nyingi zilizomkuta mpinzani wake, kulinganisha na Tinampay,” alisema.
Bondia bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Karama Nyilawila alisema mbali na Mwakinyo kushinda, lakini Watanzania wanapaswa kuwa wazalendo na ushindi huo.
“Wapo wanaosema Mwakinyo kapigwa, lakini hawajui tu mabondia wa Tanzania tukienda kucheza nje nini kinatokea kama tukimaliza raundi zote,” alisema.
Alisema katika pambano hilo, kuna raundi kweli Tunampay alionekana kumshambulia Mwakinyo lakini ni raundi chache kulinganisha na zile ambazo Mwakinyo ali shinda.
“Haijalishi umempigaje mpinzani wako katika kila raundi, hata umpige ngumi nyingi kiasi gani kama hajasalimu amri, maana yake wakimaliza raundi hiyo aliyeshinda ana pointi 10 na  aliyepigwa ana pointi tisa, hivyo zinapokuja kujumlishwa mwishoni ikaonekana Mwakinyo ana pointi nyingi sababu aliongoza raundi nyingi kulinganisha na mpinzani wake.
Bondia Mada Maugo alianza kwa kutania kwamba hata mabondia wa Tanzania wakienda kupigana nje ya nchi wanapopigwa wasiambiwe wameuza mapambano.
“Tunampongeza Mwakinyo kwa ushindi, lakini pambano lilikuwa gumu kwake,” alisema Maugo.

Kona yake ilianza kumu ogopesha mapema
Tofauti na Tinampay ambaye alihudumiwa na watu wawili pekee ulingoni, kona ya Mwakinyo ilikuwa na zaidi ya watu watano wakiongozwa na kocha wake, Hamis Mwakinyo ambaye ni kaka yake.
Kabla ya pambano hilo kuanza, mmoja wa watu waliokuwa kwenye kona ya Mwakinyo aliyejulikana kwa jina la Meter Band alianza kumpepea kitendo kilichoacha maswali kwa  mashabiki, huku mpinzani wake akiwa amekaa akisubiri muda wa pambano tu.

Raundi 10 zilivyokuwa
Mwakinyo alisubiri hadi raundi ya tatu ili kuwanyanyua mashabiki baada ya kucheza kwa kutegea kana kwamba anamsoma mpinzani wake raundi ya kwanza na ya pili amiruhusu kushambuliwa na Tinampay kabla ya kumgeuzia kibao raundi ya tatu iliyoibua shangwe la maelfu ya  Watanzania waliojitokeza kushuhudia pambano hilo huku wale wachache kutoka
Ufilipino wakiwa kimya.
Raundi ya nne, Mfilipino alionywa na refarii baada ya kupiga ngumi chini ya mkanda, baada ya kuchezea kipigo katika raundi hiyo kilichomchanganya na raundi ya tano Mwakinyo alijikusanyia pointi kwa kupiga ngumi za kudokoa na kutoka kwa haraka akimkimbia mpinzani wake ambaye muda wote hakukubali kurudi nyuma.
Dakika ya sita, Tinampay alitumia mbinu ya kumbananisha Mwakinyo kwenye kona na kumshambulia lakini Mwakinyo alijihami kwa kujikinga usoni na Mfilipino kumchapa ngumi za tumbo mfululizo kwa lengo la kumkata pumzi, lakini Mwakinyo alipuuzia ngumi hizo kwa kuchezesha kiuno kuashiria ngumi hizo si kitu kwake na kumgeuzi kibao kwa kumshambulia bila majibu na kuamsha kelele za mashabiki wakimtaka Mwakinyo amalize pambano, lakini Tinampay alichomoka na kukaa sawa kabla ya kumbananisha tena Mwakinyo kwenye kamba.
Kabla hajakaa vizuri Mwakinyo alitaka kuteleza lakini stamina ilimsaidia na kumkimbia mpinzani wake.
Raundi ya saba, Mwakinyo alikwenda chini lakini refarii alikataa si konde bali aliteleza hivyo hakumhesabia zaidi ya kumfuta glovu ingawa alimpa nafasi ya kumshambulia mpinzani wake.
Raundi ya nane, Tinampay alianza kwa kasi na kuendelea kumbananisha Mwakinyo kwenye kona, ingawa Mtanzania huyo alitumia mbinu ya kumkimbia huku akijibu mashambulizi kwa  kushtukiza na Tinampay kuendelea kumshambulia Mwakinyo ambaye aliokolewa na kengere ya muda na Mfilipino huyo kuendeleza mashambulizi raundi ya tisa.
Kushambuliwa kwa Mwakinyo kulimfanya aonekane kama kulewa jambo lililofanya mashabiki wa Tanzania waliongozwa na Waziri Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison  Mwakyembe kuwa kimya huku wachache wakipiga kelele kumtaka Mwakinyo amkimbie mpinzani wake ili amalize raundi hiyo.
Raundi ya 10, Mwakinyo aliamsha shangwe kwa mashabiki baada ya kumshambulia Tinampay kana kwamba Simba aliyejeruhiwa lakini Mfilipino huyo hakukubali kabla ya majaji wawili kutoa ushindi wa pointi 97-93 na 98-92 kwa Mwakinyo na jaji mmoja kutoa sare ya pointi 96-96.

Mfaume, Keis wawagawa mashabiki
Pambano la utangulizi kati ya Mfaume Mfaume na Keis Ally liliwagawa mashabiki waliofurika uwanjani hapo.
Licha ya Mfaume kutangazwa mshindi kwa pointi za majaji 3-0, mashabiki wa Keis wala hawakuumizwa na matokeo hayo kutokana na rekodi ya bondia huyo anayetokea kambi ya Manzese ambaye juzi alipigana pambano lake la nne kwenye ngumi za kulipwa kulinganisha na Mfaume ambaye ni mkongwe.
Raundi ya nane na ya mwisho ndiyo ilimbeba Mfaume anayetoka kambi ya Manzese ambaye alimpeleka chini Keis kwa ngumi kali ya kulia iliyompata sawia usoni na kumpeleka chini huku akimwacha Mfaume akimwonyesha ishara ya kumkebehi kwa kucheka kwa jeuri akimfuata kabla ya refarii, Anthony Rutta kumuonya kwa kumtaka arudi kwenye kona yake kabla ya  kwenda kumhesabia Keis ambaye alinyanyuka fasta na kuendelea na pambano Majaji, Neneko Abdallah na Pendo Njau walitoa pointi 78-74 kila mmoja wakati Mlundwa  akitoa ushindi wa pointi 79-72 kwa Mfaume ambaye alitwaa ushindi kwa pointi za majaji 3-0.

Hawa waliweka heshima ya TKO
Said Chino na Twaha Kiduku waliweka heshima ya kushinda kwa matokeo yasiyokuwa na ubishi  ya ushindi wa Technical Knock Out (TKO) katika mapambano ya utangulizi.
Chino alimchapa Mohammed Bakari kwa TKO raundi ya nne ya pambano lililokuwa la raundi sita huku akimpeleka chini mara mbili.
Twaha alimchapa France Ramabolu wa Afrika Kusini kwa TKO raundi ya tano huku Msauzi huyo akiokolewa na mwamuzi baada ya kupigwa ngumi zaidi ya 10 mfululizo bila majibu.
Pambano jingine, Loren Japhet alichapwa na Salim Jengo kwa pointi za majaji 3-0, Hemed Mrema alishinda kwa matokeo kama hayo dhidi ya Azizi Juma na Juma Athuman alimchapa Bob Brown katika mapambano ya utangulizi.

Mashabiki waweka historia
Achana na historia ya mashabiki wa ngumi kuujaza uwanja wa Uhuru kushuhudia pambano hilo, lakini katika kuonyesha mapenzi yao kwenye mchezo huo, mashabiki walianza kujitokeza  uwanjani saa 2 asubuhi wakisubiri pambano ambalo awali lilielezwa kuanza saa 12.30 jioni lakini lilianza saa 1.30 usiku kwa mapambano ya utangulizi kabla ya lile la Mwakinyo lililoanza saa 5.25 usiku.
Mashabiki hao ambao walizuiwa nje ya uwanja wakitakiwa kusubiri muda walionyesha subira hadi saa 9 alasiri ambapo mageti yalifunguliwa huku kiingilio kikiwa bure na kujaza robo tatu  ya majukwaa ya Uwanja wa Uhuru, huku mashabiki wa VVIP na VIP pia wakijaza viti hivyo na wengine kulazimika kukaa chini.