Kijiweni live: Kumbe Dogo Aslay ana busara kuliko Stamina

Tuesday January 14 2020

Mwanaspoti-Kijiweni live-Kumbe-Tanzania-Dogo Aslay-ana busara- kuliko-Stamina-Mwanasport-Michezo

 

By Luqman Maloto, Dk Levy

KIJIWENI leo kuna mjadala wa nyimbo mbili, “Naenjoy” wa Aslay na “Asiwaze” wa Stamina. Kila mmoja aliimba baada ya kutendwa kimapenzi. Nani kaua kuliko mwenzake? Yupi katumia busara kumzidi mwenzie. Bunge la kitaa lipo live na wabunge wa kijiweni Luqman Maloto na Dk Levy.
LUQMAN: Oyaa mwana, kitu Asiwaze. Stamina kakomesha.
DK LEVY: Kitu Naenjoy. Mwanangu Aslay alionyesha ukomavu kwenye mapenzi. Stamina analialia, Aslay anatuma taarifa kuwa yeye anaenjoy maisha, hakuna kilio wala mateso.
LUQMAN: Msikilize Stamina alivyokung’uta kona zote. Kaacha nini? Halafu anamwambia shem kuwa kule alipo Asiwaze. Kwake hajaacha pengo kabisa.
DK LEVY: Angekuwa hajaacha pengo angelilia mpaka suti aliyovaa wakati wa kufunga ndoa? Keki alikata ya nini? Michango alichangisha ya nini? Mshenga alimtuma wa nini? Pengo lipo ndio maana anaapa mpaka akifa msibani asiende.
LUQMAN: Mtu akisema suti alivaa ya nini ndio kuthibitisha kwamba kwake kuna pengo? Wewe sijui huwa unatumia kifaa gani kufikiri na kupata majibu. Anaposema kile kiapo aliapa kwa nini? Mahari alilipa kwa nini? Au keki alikata ya nini? Ni kufikisha ujumbe kuwa alifanya kitendo ambacho leo hii anaona ni cha kipuuzi. Ndoa yote kaipuuza na leo yupo shwari.
DK LEVY: Utatetea uwezavyo, yule Stamina ana donge limemkaba. Wewe mwanamke mzuri mzuri vile halafu dogo wa Simba kapita naye kwa spidi ya drone za kivita kama iliyomuua Jenerali Qassem Soleimani, unadhani ataacha kunung’unika? Halafu unachukiaje mapenzi kwa sababu ya mwanamke mmoja, si umkaribishe mwingine azibe pengo? Aslay ndio mjanja, yeye haweki vinyongo anasema anaenjoy zake.
Msikilize Aslay anasema kwenye Naenjoy “Maisha ni yaleyale kuteswa ni kama funzo. Mengine tuyasamehe, tusiweke viulizo. Kikubwa uhai nashukuru ninao, sijakufa. Ila kuhusu mapenzi sitaki shobo, nimeyakuta.” Aslay fundi sana, ameongea mazito. Stamina alijifanya mapenzi anayaweza, ndio maana anamwaga machozi yote. Aslay anasema mapenzi kayakuta, hataki shobo.
LUQMAN: Mbona humalizii line ya Aslay kuwa “mapenzi yana wenyewe, sisi wengine tuache shobo, tutazikana wazimawazima” na aliposema “jamani shuka zina joto lake asikwambie mtu kitu chochote. Kugandanagandana, kuzuga tunapendana, mwisho tunaanza kulizana, sitaki. Mi na sizitaki nyama, kupenda nimesimama, moyo wangu umegoma, hautaki tena, ng’o.” Hapo Aslay anacheka? Analia kwenye verse halafu kiitikio anajidai anaenjoy. Kwa kifupi, Stamina amemaliza kesi kibabe, Aslay analeta unyonge.
DK LEVY: Tofautisha unyonge na busara. Aslay ana busara, sikiliza mstari “Ulemavu wa kichwa ukanipa magongo”. Mtu anaumwa kichwa, unampa magongo atembelee si dharau hizo? Aslay anasema yeye anaenjoy, maisha ni yaleyale lakini yupo poa. Yale magongo aliyompa katika ulemavu wa kichwa, aliyapuuza, sasa anajitibu kichwa mwenyewe.
LUQMAN: Acha mistari ya kinyonge wewe. Hebu sikiliza hii punchline “Kama ni pete nisharudisha kwa sonara, tayari nishavuta mpunga, nimerudisha nusu hasara.” Na hii nyingine “hiki cheti cha ndoa, nimebaki nacho kwa nini, siwezi kuombea kazi, hakina mchongo hapa mjini.” Hapo inatoka mistari yenye nguvu. Kwa kifupi Stamina halilii ndoa ila anaisimanga ndoa. Anausimanga uhusiano wake na shemeji yetu ndio maana anabomoka kuwa “ndoa ndoano anayebisha aniulize mimi, nilishakuwa na mahusiano ambayo sijui hata yanahusiana na nini.”
DK LEVY: Tofauti ya Aslay na Stamina ni busara. Aslay ameonyesha busara za kiwango cha juu, ndio maana anasema mambo mengine ni ya kusamehe, kikubwa uhai. Stamina hataki hata azikwe. Hivi huyo Stamina angekutana na aliyokutana nayo Aslay je? Tuliofahamu kilichokuwa kinaendelea tulidhani Aslay muziki ndio basi tena. Hata hivyo, alitulia na kuibuka na ‘Naenjoy’, ungekuwa una akili, ungekuwa umeshaniuliza kwa nini Aslay hakusainiwa WCB. Ya Aslay ni mazito.
LUQMAN: Hiyo stori yako kuhusu Aslay itunze labda itakupa faida siku za usoni. Aslay hata yawe yamemtokea yapi, hayawezi kufikia ya Stamina. Yule ni mke wa ndoa kabisa. Ndio maana kwenye Asiwaze, anasema ndoa aulizwe yeye. Yule Aslay kesi yake haijahusisha michango ya ndugu na marafiki wala wasimamizi wa ndoa. Kwa hiyo usithubutu kulinganisha kesi ya Stamina na Aslay, hazikaribiani. Ugomvi wa mahawara hauwezi kuwa sawa na wa wanandoa.
DK LEVY: Hao ndugu zako wa Simba, walikutana na Yanga Uwanja wa Taifa, mechi yenye faida, walitakiwa kupata pointi tatu za kuupata ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakapata mabao mawili ya kuongoza, wakashindwa kulinda ushindi, mechi ikaishia 2-2. Sasa hivi wanakuja na stori eti Yanga waliwakimbia Mapinduzi Cup. Ni wazima hao kweli?
LUQMAN: Simba wana akili timamu wewe, walitaka wakutane na Yanga Mapinduzi Cup ili Yanga watoe majibu ile sare ya 2-2 Taifa walipataje? Ile mechi haikuwa ya Yanga kupata hata on target moja, achilia mbali kupata goli. Simba walishangazwa, ndio maana walitaka Yanga watoe majibu walipataje droo Taifa? Kisha Simba wangebeba ubingwa Mapinduzi Cup na kumpa kichapo Yanga.
DK LEVY: Kwani Simba walidanganywa kuwa Mapinduzi Balama asingecheza Mapinduzi Cup? Walidhani Mo Banka na Haruna Niyonzima wasingecheza? Kwa kifupi Simba wanapaswa kuwashukuru Mtibwa kuifunga Yanga nusu fainali Mapinduzi Cup, vinginevyo Yanga wangeichapa Simba, ndio watu wangejua kuwa Simba bila maneno ya Haji Manara ni sawa na paka koko.
LUQMAN: Na ndicho Simba walitaka wamuone huyo Mapinduzi Balama kama angepiga tena shuti kulenga goli, wamuone Niyonzima na Mo Banka kama wangecheza mpira wao tena. Kwa kifupi mimi sisemi kama Yanga waliikimbia Simba, ila walijilegeza mno kwa Mtibwa dakika za mwishoni mpaka Mtibwa wakarudisha goli. Halafu wakafungwa penalti. Kama sio kuikimbia Simba ni nini?
DK LEVY: Na huko Simba ndipo kuna chanzo cha mgogoro wa ndoa ya Stamina. Na Stamina haipendi Simba ‘ova his dedi bodi’. Yule mchezaji wa Simba aliyetembea na mke wa Stamina ndio kasabisha hasira za Stamina kwa Simba. Inawezekana mnalia yale magoli mawili kurudi kimiujiza, kumbe Simba inatafunwa na laana ya Stamina. Hapohapo hatujaanza kuzungumzia ile nyingine inayohusu rambirambi za Mafisango.

Advertisement