Kenya yanusa medali, Tanzania yasubiri ya nusu fainali Tenisi Afrika

Wednesday January 8 2020

Mwanaspoti-Kenya-yanusa medali-Tanzania-yasubiri-nusu fainali- Tenisi Afrika

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Wakati wenyeji Tanzania wakisubiri matokeo ya wachezaji wake watatu katika michezo ya baadae leo ili kujihakikishia medali, Kenya imekuwa nchi ya kwanza kujihakikishia medali kwenye mashindano ya Tenisi Afrika Mashariki na Kati yanayoendelea kwenye viwanja vya klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam.

Katika mashindano hayo, Watanzania, Rashid Ramadhan atakayecheza na Manishimwe Emmanuel wa Rwanda, Naitoti Singo atakayemkabiri Melisa Mwakha wa Kenya na Kanuti Alagwa atakayecheza na Mussa Kashindi wa Burundi, wanahitaji ushindi  katika mechi zao za leo za nusu fainali ili kujihakikishia medali hata kama watafungwa kwenye fainali kesho Alhamisi.

Wakati Watanzania hao wakisubiri matokeo ya mechi za leo, Kenya ina uhakika wa medali mbili mpaka sasa licha ya kusubiri mechi za nusu fainali baadae mchana huu.

Kenya imeingiza wachezaji watatu kwenye hatua ya nusu fainali kwa wasichana chini ya miaka 16, ambao mmoja ana uhakika wa kufuzu kucheza fainali huku mwingine akisikilizia matokeo ya mechi ya nusu fainali ya pili.

Wachezaji hao ni Alicia Awegi atakayemkabiri Roselida Asumwa na Angella Akutonyi atakayecheza na Arielle Horpinitch wa Shelisheli.

"Tunaamini tutafanya vizuri na kuchukua medali zote tatu kwa wasichana," alisema Angella ambaye ni mchezaji namba moja kwenye mashindano hayo kwa wachezaji wa umri wake.

Advertisement

Kenya pia imeingiza wachezaji wawili kwenye nusu fainali kwa wachezaji wa kike wa umri chini ya miaka 14.

Melisa Mwakha atachuana na Naitoti wa Tanzania wakati Faith Urasa akimkabiri Carine Nishimwe wa Rwanda.

Upande wa wavulana, Manishimwe Emmanuel wa Rwanda atamkabiri Ramadhan Rashid wa Tanzania na Hakuzumwani Junior wa Rwanda atamkabiri Gatoto Allan wa Burundi.

 

Advertisement