Kenya yaimaliza Ethiopia dakika 10 za mwisho Chalenji

Sunday November 17 2019

Mwanaspoti-Kenya-yaimaliza-Ethiopia-dakika-mwisho-Chalenji-Tanzania

 

By DORIS MALIYAGA

Dar es Salaam.Mabao mawili yaliyofungwa ndani ya dakika 10 za mwisho, ziliwafanya Kenya waibuke na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa Kundi B wa Kombe la Chalenji Cecafa uliopigwa Uwanja wa AzamComplex nje kidogo ya Dar es Salaam.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulishuhudia dakika za 10 za mwisho Kenya ikipata ushindi baada ya kupata penalti iliyotolewa na mwamuzi Jonesia katika dakika ya 80.

Penalti hiyo ilifungwa na Jentrix Shikangwa na baada ya dakika moja, Cynthia Musungu alipachika la pili dakika ya 81.

Kocha Mkuu wa Ethiopia, Birhanu Gizaw hakuongea maneno mengi zaidi ya kusema, mwamuzi Jonesyia ndiye alimaliza mchezo.

"Naweza kusema, mwamuzi ndiye alimaliza mchezo kwani tumefungwa mabao ndani ya dakika 10 za mwisho za mchezo na penalti ndio ilituondoa mchezoni,"alisema Gizaw.

Kocha wa Kenya, James Ouma amefurahi kwa mchezo: "Tunafurahi kwa ushindi imekuwa bahati kwetu, hivyo ndivyo mchezo ulivyo."