Mwanariadha Cheruiyot kufukuzia rekodi dunia 2020

Thursday January 02 2020
Kenyarpic

NYOTA anayejitahidi kurithi mikoba yake bingwa wa mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop, Timothy Cheruiyot katangaza kuwa mwaka huu utakuwa wa kukimbizana na rekodi ya dunia.
Rekodi ya dunia katika kitengo hicho kwa wanaume imedumu kwa miaka 21 toka ya zamani ilipovunjwa na mpya kuwekwa 1998 na mwanariadha mstaafu Hicham El Guerrouij kutoka Morocco.
Mbio hizo huhusisha mizunguko mitatu na robo ya mita 400. Guerrouj alitumia sekunde 55 kwa kila mzunguko kuvunja rekodi ya zamani na kuweka mpya ya dakika 3:26.00 kule Rome, Italia.
Sasa Cheruiyot anayejitahidi kuvalia viatu vya Kiprop  baada yake kupigwa marufuku ya miaka nne kwa kosa la kutumia pufya, kasema mwaka huu ataandaa mikakati na maandalizi mazuri kuhakikisha  anafuta rekodi hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miongo miwili.
Cheyuiot aliaga mwaka uliopita kwa kushinda nishani yake ya kwanza ya dhahabu kwenye mbio za World Championships kule Doha, Qatar.
Mawazo yake sasa yapo kwenye Olimpiki za Tokyo, mwaka huu ambapo anawazia sio kushinda tu nishani nyingine ya dhahabu bali pia kuivunja rekodi ya dunia.
“Najua rekodi hiyo imedumu kwa muda mrefu na ili kuifuta tutahitaji mikakati  mipya pamoja na mpango kazi tofauti. Hili lipo katika mawazo yangu na huu mwaka nitaanza mikakati hiyo,” kasema.
Cheruiyot kawa kwenye mabishano mazito na mwenzake Elijah Manangoi kuhusu ni nani mbabe  mwenye uwezo wa kuichukua nafasi yake Kiprop.
Baada ya Manangoi kutawala sana mbio hizo, Cheruiyot alimgeuzia huko Doha na  pia kwenye mashindano ya Diamond League.
Wawili hao hufanya mazozi pamoja na ndio kwa sasa nyota wenye njia ya wazi  ya kumrithi Kiprop.

Advertisement