Kajala, mwanae wajitosa kusaidia watoto wa kike

Muktasari:

Kajala ni miongoni mwa wasanii maarufu nchini ambaye amewahi pia kuungana na wakurugenzi wa Gerirwa General Supplies kutoa msaada kwa timu ya Taifa ya soka ya wanawake.

Dar es Salaam.Msanii wa Bongo Muvi, Frida Masanja ‘Kajala’ na mwanae Paula wamejitosa kwenye kampeni ya Rani na Binti Shuleni inayolenga kusaidia wanafunzi wanaotokea kwenye familia duni nchini kupata bure pedi za Rani.

Kampeni hiyo ya miezi sita imezinduliwa Leo Ijumaa jijini Dar es Salaam huku Kajala akitajwa kuwa balozi wa pedi hizo.

"Nafarijika kuingia katika kampeni hii kwani mimi ni mama wa watoto wengi licha ya kwamba Paula ndiye anajulikana," alisema Kajala.

Alifafanua kwamba kama mzazi, mwanae huyo wa kike ana marafiki zake ambao yeye anawachukulia kama watoto wake pia.

Akizungumzia kampeni ya Rani na binti shuleni, Kajala alisema ataitendea haki katika kuwasaidia mabinti wa kike wanaotoka kwenye familia duni kutokosa masomo kwa kukosa pedi wanapokuwa kwenye hedhi.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Gerirwa General Supplies, Hawa Hassan alisema kampeni hiyo ya miezi sita itasaidia kugawa pedi za Rani kwa wanafunzi wa kike kwa baadhi ya shule zenye uhitaji mkubwa nchini.

Alisema kampeni hiyo itaanza Januari hadi Juni na baada ya hapo wataangalia utaratibu wa kuendelea kuwasaidia wanafunzi wa kike wenye changamoto ya kukosa masomo wanapokuwa kwenye hedhi kwa kukosa pedi.