KMC yawasimamisha Katibu Mkuu, Afisa habari kisa vipigo

Muktasari:

KMC ipo nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo 16 ikishinda michezo mitatu, kutoka sare mara tano na kukubali kipigo katika michezo nane.

Dar es Salaam. Uongozi wa klabu ya KMC umewasimamisha kazi Katibu Mkuu wake Wolter Halson na Afisa Habari, Anuary Binde kupisha uchunguzi wa matokeo mabaya wanayoyapata ya timu hiyo.

KMC ipo nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo 16 ikishinda michezo mitatu, kutoka sare mara tano na kukubali kipigo katika michezo nane.

Mwenyekiti wa Bodi KMC, Meya Benjamini Sitta alisema ni kweli wamewasimamisha lengo ni kupisha uchunguzi hivyo hawatakuwa wakihusika kufanya majukumu yoyote ndani ya klabu hiyo.

Alisema uamuzi waliouchukua ni kutokana na sababu ambazo zipo ndani ya uwezo wao kwasasa hawawezi kuzungumza lolote hadi hapo watakapokamilisha uchunguzi wao huo.

Katika hatua nyingine Sitta alisema klabu hiyo imemalizana na wachezaji Vitalis Mayanga, Alon Lulambo na Melly Mongolare na kuthibitisha kuwa chanzo cha kufanya hivyo ni kupunguza gharama.

"Kuna wachezaji tumeamua kuachana nao ili kupunguza matumizi kuhusu suala la usajili hadi muda utakapokwisha kila mmoja atafahamu ni mchezaji gani kasajiliwa kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye klabu yetu," alisema Sitta.