Jicho la Mwewe: Mastaa wa Yanga wanapokimbia maisha halisi

Muktasari:

Kuna wanasiasa waliingia kuchanga na kuwavuruga zaidi Wanayanga kwa kuendelea kuwaimbisha huu usemi wa ‘Timu ya Wananchi, wawekezaji ni wananchi’. Wanasiasa walichanga kidogo kisha wameondoka zao.

BARUA za mastaa wa Yanga kuvunja mikataba zinasikitisha. Unasoma halafu unasikia imani. Kwa miezi mitatu, miwili hawajalipwa mishahara. Walikuwa wanaishije? Mungu anajua. Hawa wachezaji wa kigeni kwao ilikuwa tabu tupu.
Anko Mrisho Ngassa anaweza kuingia mtaa huu akatokea mtaa mwingine akajikuta ana Sh200,000. Vipi kwa Lamine Moro? Ni ngumu. Na sasa mastaa wa kigeni wa Yanga wameamua kuvunja mikataba yao na kuondoka.
Ni mwendelezo wa hadithi ya Yanga mpya. Yanga ya baada ya kuondoka kwa Yusuph Manji. Hakuna kinachoeleweka pale Jangwani. Wakati akiwa madarakani kuna watu walikuwa wanampinga Manji. Sasa hivi na wao wametokomea.
Hawa ndio wale waliokuwa wanasema ‘Yanga ni kubwa kuliko Manji’. Tuliwakubalia. Kuna wengine wakawa wanasema ‘Atuachie Yanga yetu’. Tukawakubalia. Kuna wengine waliokuwa wanasema ‘Ananufaika na Yanga’. Tukatikisa kichwa juu tukiwakubalia.
Kuna wengine walikuwa wanasema tajiri wa Afrika Aliko Dangote alikuwa tayari kuwekeza Yanga. Tuliwakubalia. Leo wachezaji hawana mishahara. Dangote hatumuoni. Wale wawekezaji ambao, tuliambiwa wangekuja pindi Manji akiondoka hatuwaoni.
Uongozi mpya wa Yanga ulipoingia madarakani ikapitishwa harambee ya uhakika. Zikapatikana zaidi ya Sh 500 milioni. Nijua kwamba yalikuwa maigizo ya muda tu. Hizo pesa ni bajeti ya mwezi mmoja tu kwa Yanga. Nilijua kwamba maisha halisi ya Yanga yangerudi. Na sasa yamerudi kweli. Wachezaji wanavunja mikataba hawana mishahara.
Kuna wanasiasa waliingia kuchanga na kuwavuruga zaidi Wanayanga kwa kuendelea kuwaimbisha huu usemi wa ‘Timu ya Wananchi, wawekezaji ni wananchi’. Wanasiasa walichanga kidogo kisha wameondoka zao. Wameiacha Yanga pale pale katika mfumo uliofeli wa miaka yote. Mfumo wa kuendeshwa na wanachama.
Viongozi wapya wa Yanga walipoingia walipaswa kufanya mambo mawili. Kwanza ni kuipeleka timu katika muundo tofauti. Muundo mwingine. Muundo wa hisa. Mwenye kisu kikali ale nyama. TP Mazembe kuna Moise Katumbi, Mamelodi Sundowns kuna Motsepe, Kaizer Chief kuna Kaizer Motaung, Simba kuna Mohamed Dewji, Chelsea kuna Roman Abramovich. Yanga kuna nini?
Mfumo wa timu kuendeshwa na wanachama Yanga umefeli. Nilidhani kwamba viongozi wangeogopa deni la kuongoza klabu katika zama hizi. Hizi ni zama za matumizi makubwa ya pesa katika mpira. Hizi sio zama za kumnunua mchezaji kwa kumpa feni ya ukutani. Sio zama za kumlipa mchezaji maneno badala ya pesa.
Viongozi badala ya kujikita katika kuandaa mabadiliko ya mfumo wao wamejikita katika kuchagua kamati mbalimbali ambazo hazina tija klabuni. Kamati za uongo uongo ambazo haziwezi kufanya lolote bila ya kitu kinachoitwa pesa.
Timu kubwa kama Yanga haiwezi kwenda kwa michango. Kama si kumtupia mzigo tajiri basi viongozi walipaswa kuandaa mifumo madhubuti ya kuifanya Yanga iishi kwa jina lake. Hata hivyo, imekuwa wimbo kuifanya Yanga ijitegemee. Kinachosemwa na kinachoweza kufanyika ni mambo tofauti kabisa.
Yanga haiwezi kuishi kwa pesa za SportPesa, Vodacom, Azam na mapato ya mlangoni pekee. Kunahitajika ubunifu wa hali ya juu kuweza kupata pesa za kuisafirisha timu kila mahala, kuiweka hoteli nzuri na kuwalipa mishahara wachezaji.
Inawezekana Simba bado hawajafanikiwa, lakini naamini wapo katika mfumo sahihi. Inawezekana labda baadaye mwekezaji wao akaonekana sio mtu sahihi, lakini hawapaswi kurudi nyuma. Inabidi wabakie katika mfumo huo huo na labda wabadili mwekezaji tu.
Hili la Yanga kubakia katika mfumo uliopo na kudanganyana kuchanga pesa kwa kutumia wanasiasa lilishafeli kwa miaka mingi. Hauwezi kutembeza bakuli kila mwezi. Umefika wakati sasa kwa wafanyabiashara wenye pesa nyingi kuwekeza katika Yanga.
Umefika wakati sasa watu wenye biashara zao kujinufaisha kupitia Yanga kihalali na kisha kuinufaisha klabu yenyewe. Haiwezekani kila mwenye Yanga akawa na sauti ndani ya klabu kwa sababu ya mchango wa Sh 10,000 kwa mwaka. Wapi na wapi!
Hesabu za vidole kwamba ‘mashabiki 200,000 Yanga wakichanga Sh. 10,000 kila mwezi zitapatikana Sh 2 bilioni’ zimepitwa na wakati. Hizi ni hesabu rahisi katika mdomo, lakini haina uhalisia pale utakapoamua kutembeza bakuli lenyewe. Mashabiki hawatoi na wenyewe pia wana shida zao huko majumbani.
Mfumo wa kudanganyana kwamba Barcelona na Real Madrid zinaendeshwa na wanachama pia ni ujinga. Waangalie mfumo mzima na wagundue kwamba, Florentino Perez amewekeza mabilioni ya pesa katika klabu yake. Ni mtu tajiri ambaye anaiongoza klabu kibiashara zaidi na sio kupitia michango ya wanachama.
Yanga waache kujidanganya na warudi katika dunia halisi ya soka la kisasa. Vinginevyo klabu yao itaendelea kuangamia kila kukicha kwa kuendekeza vyeo vya ‘Mwenyekiti’, ‘Makamu Mwenyekiti’, ‘Kamati ya Utendaji’ na vyeo vingine.
Ukiondoka uongozi uliopo na kisha ukaja uongozi mwingine wa mfumo huu huu bado haitasaidia. Mambo yatakuwa yale yale tu. Kinachopaswa kubadilika ni mfumo mzima wa namna ya kuiendesha Yanga na hapo hutaona tena bakuli mitaani.