Harmonize kuwachezesha Uno Mtwara, Diamond kuwaimbisha Baba lao Kigoma

Muktasari:

Mashabiki wa burudani kutoka Kanda ya Kusini na Kati watashuhudia burudani ya kukata na shoka kutoka kwa wasanii waliowahi kuwa katika lebo moja (WCB) Harmonize na Diamond ambao kila mmoja ameamua kwenda kwao kutoa shukurani kwa mashabiki wake.

Dar es Salaam. Miaka saba iliyopita Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa lebo ya WCB, Diamond Platnumz alitua na helikopta maeneo ya Mbagala, Dar es Salaam katika ukumbi maarufu wa Dar Live ambako alifanya shoo ya aina yake na kwa mara ya kwanza alisikiliza uimbaji wa Harmonize na kumchukua mazima.

Leo Jumanne ya Desemba 31, 2019 Harmonize naye anatua na helikopta katika viunga vya mkoa wa Mtwara ambapo mbali ya kuwasalimia mashabiki wake na kutoa shukurani atafanya ya kwanza ya aina yake tangu atoke katika lebo ya WCB na sasa yeye ni CEO wa lebo ya Konde Gang.

Shoo hiyo aliyoipa jina ‘HarmoNightFest' itafanyika Tandahimba ambapo atafanya vitu kadhaa kabla ya shoo  ikiwa ni pamoja na kugawa nguo zake bure alizovaa katika shoo mbalimbali ambazo kwa msanii ni ngumu kuzirudia tena majukwaani.

Wakati Konde anajipanga kwa shoo hiyo ya kwanza kubwa akiwashukuru mashabiki wa nyumbani kwao Mtwara, aliyekuwa bosi wake Diamond anayetamba na wimbo la ‘Baba lao’ naye yupo nyumbani kwao mkoani Kigoma akitoa shukurani kwa mashabiki wa mkoa huo.

Ambapo mbali ya shoo hiyo amezindua msikiti alioujenga mjini Kigoma, madrasa na anamalizia ujenzi wa kisima.

Diamond pia atafanya shoo usiku wa leo katika uwanja wa Lake Tanganyika, ambapo mashabiki aliotoka nao Dar es Salaam kwa treni na wa mkoani humo wataingia bure kushuhudia shoo hiyo ya kufunga mwaka 2019.

Kwa upande wa Harmonize hii itakuwa shoo ya pili Mtwara ukiachilia ile aliyoifanya akiwa na WCB, iliyopewa jina la ‘Twenzetu tukaijaze Nangwanda Sijaona’.

Harmonize anayetamba na wimbo wake wa Uno pamoja na uchanga wake bado anajitahidi kutumia ujuzi alioupata akiwa na WCB, ikiwa ni pamoja na kupanga shoo anapokuwa jukwaani.

Mpangilio wa mavazi, jinsi ya kucheza anapokuwa jukwaani na kutumia madansa wengi, kama ambavyo alifanya alipokuwa akitumbuiza katika tamasha la muziki mnene ambapo alipanda jukwaani na kiti kama mfalme.

Hii itamfanya aendelee kuwa midomoni mwa watu kwa sababu anajua kuteka hadhira ya watu kila anapofanya jambo ni kupita.

Mashabiki wa burudani wa nyota hao wa Bongofleva kutoka Kanda ya Kati na Kusini watashuhudia burudani safi ya kufungia mwaka usiku wa leo.