Hakuna kombe wala ganji kwa bingwa wa Ligi Kuu Kenya

Saturday January 11 2020

Mwanaspoti-Hakuna-Kenya-Gormahia-kombe-wala ganji-bingwa-Ligi Kuu Kenya

 

By THOMAS MATIKO

NI kungori arif. Si ati nini, maisha kwenye Ligi Kuu ya KPL tayari ni magumu na bado tu. Kulingana na mwenyekiti wa KPL ambaye pia ni mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier, hali itaendelea kuwa mbaya katika ligi hiyo hadi pengine mwisho wa msimu.
Na sio hiyo tu, timu itakayoibuka bingwa haitapata fedha zozote wala taji maana hazipo. Msoto umetawala na KPL hawana ujanja ila kuzikayagia. Imekuwa utaratibu kama tu kokote kwingine duniani, kwa bingwa wa KPL kutunukiwa kombe pamoja na Sh4.5 milioni kila mwisho wa msimu, lakini sasa hiyo itabaki kuwa stori.
Toka Sportpesa ilipofunga duka na kusitisha udhamini wake wote, bodi inayoendesha Ligi Kuu imekuwa ikijitahidi kupata mdhamini mpya lakini ni kama vile wamesare baada ya kushindwa kumpata.
Ambrose kawa muwazi na kukiri kwamba kwa sasa KPL haina matumaini kabisa ya kupata mdhamini wa kuifadhili Ligi Kuu.
“Kikweli mambo sio mazuri kwenye ligi ya KPL na sioni hali ikibadilika. Hamna dalili zozote za kumpata mdhamini mpya msimu huu na pengine hata kuendelea. Wadhamini  tuliofanikiwa kupata mpaka sasa wamekuwa wakijitoa kwa sababu mechi zetu hazipeperushwi laivu au kwenye vituo vya kimataifa. Ndio hali tunayopitia kwa sasa inasikitisha lakini tufanyeje,” Rachier kafunguka.
Lakini hata bado Rachier anasema kwa wadhamini hao waliofanikiwa kufanya mazungumzo nao, wanaganda kutoa pesa za maana kutokana na kuwa ligi ya KPL haipeperushwi hasa kwenye chaneli za kimataifa.
Sportpesa walipokuwepo walitoa hela ijapokuwa biashara yao ilikuwa ya kubeti. Kabla yao KPL ilifurahia maisha chini ya Supersport ambayo ni chaneli ya kimataifa na mechi za KPL ziliweza kurushwa chaneli hiyo. Hata hivyo Supersport nao walifunga duka hasa baada ya Rais wa sasa wa Shirikisho la soka nchini Nick Mwendwa kulazimishia ligi kuwa na timu 18 badala ya zile 16. Supersport walikuwa mmoja wa wadau waliopinga upanuzi wa ligi na ni baada ya kupanuka kwa ligi ndipo wakajitoa.
Hawa ndio wadhamini wa pekee ambao waliweza kutoa fedha za maana kuifadhili ligi ya KPL kwa mujibu wa Rachier. “Kwa wadhamini tuliowapata kama watatu au wanne hivi, kiasi cha fedha za usajili ambacho wamekuwa wakipendekeza ni kidogo sana kufadhili ligi. Na hii ni kwa sababu hiyo ya kwamba mechi zetu hazipeperushwi kimataifa”
Kutokana na msoto huo ndio sababu bingwa wa msimu huu atatoka kavu. Hatapata chochote ganji wala kombe sababu KPL haina hela. Kombe la mwisho waliondoka nalo kabisa Gor baada ya kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo mwishoni mwa msimu uliopita.
Hali imekuwa mbaya hivyo kiasi kuwa hata KPL imelazimika kuhama kwenye afisi zake mtaa wa kifahari kule Westlands na kuhamia Lenana Road ikiwa ni kupunguza matumizi.

Advertisement