Gofu kuanzisha mashindano ya kumuenzi Mufuruki

Muktasari:

Mwakilishi wa Club ya Golf, Brigedia Mstaafu Michael Luongo amesema Club hiyo itaanzisha shindano litakaloitwa Ali Troff Golf ili kumuenzi.

Dar es Salaam. Mwakilishi kutoka Club ya Golf, Brigedia Mstaafu Michael Luongo amesema Club hiyo itaanzisha shindano litakaloitwa Ali Troff Golf ili kumuenzi Marehemu Ali Mufuruki aliyekuwa mwanachama wao tangu mwaka 2007.

Brigedia mstaafu Luongo amesema Desemba 7 mwaka huu kulikuwa na shindano la mwisho wa mwaka ambalo hata hivyo Mufuruki hakuhudhuria.

"Tulishangaa wakati tunajiandikisha majina hatuoni jina lake, kitu ambacho siyo kawaida yake, licha ya kuwa na majukumu mengi hakuwahi kupitisha siku mbili bila kuja kwenye mazoezi kumbe mpendwa wetu alikuwa anaumwa,"amesema.

Mufuruki alijiunga katika club hiyo 2007, mwaka ambao club hiyo ya jeshi ilianzishwa hivyo amesema alikuwa kama mmoja wa waanzilishi.

Amesema watamkumbuka kwa ucheshi wake bila kujali hadhi yake na alitengeneza chumba maalumu kwa ajili ya kubadilishia nguo kwa upande wa wanaume.

"Alikuwa anapenda sana golf na siyo tu kucheza bali alitaka kila mtu mtu ajue sheria ya mchezo huo, kwa hiyo ratiba itapangwa ya lini shindano hilo lifanyike," amesema.

Mufuruki alifariki dunia Desemba 8, 2019 nchini Afrika ya Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu atazikwa makaburi ya Kisutu saa 10:00 jioni.