Eymael afunguka siri ya Molinga kubaki Yanga

Muktasari:

Eymael alisema baada ya kuwasikiliza mabosi zake kuhusu tuhuma za Molinga, aliwaomba kufuta mpango wa kuachana naye huku akiamini, adhabu hiyo ni kubwa kwa mchezaji ambaye ana uwezo uwanjani.

MASHABIKI wa Yanga hawakuwa wakielewa sababu za mabosi wa klabu hiyo kutaka kumtema mpachika mabao wao, David Molinga a.k.a Falcao.
Tayari Molinga aliondoka nchini kurejea Ufaransa huku uongozi wa Yanga kupitia Ofisa Habari wake, Hassan Bumbuli ukiweka hadharani kuwa ni miongoni mwa mastaa wa kigeni watakaotemwa kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Alhamisi usiku.
Hata hivyo, habari kutoka ndani zinasema kuwa mpango wa kuachana na Molinga, ambaye ameifungia Yanga mabao manne umekwama baada ya kocha mpya, Luc Eymael kuzuia na kuagiza arudishwe kikosini na hilo tayari limetelekezwa na Mkongomani huyo juzi kuanza kufanya mazoezi na wenzake katika Viwanja vya Chuo cha Sheria, Dar es Salaam.
Eymael alisema wakati anatazama video za mechi mbalimbali za Yanga alivutiwa na staili ya upambanaji ya Molinga.
Hata hivyo, alisema alishangazwa kwani baada ya kutua nchini na kukamilisha dili la kuinoa Yanga, hakumuona mchezaji huyo ndipo akawauliza mabosi zake kuhusu Molinga.
Katika kuuliza akajibiwa kuwa alikuwa mbioni kutemwa kweye dirisha dogo la usajili kutokana na matatizo ya kinidhamu.
Eymael alisema baada ya kuwasikiliza mabosi zake kuhusu tuhuma za Molinga, aliwaomba kufuta mpango wa kuachana naye huku akiamini, adhabu hiyo ni kubwa kwa mchezaji ambaye ana uwezo uwanjani.
“Baada ya taarifa hiyo nilijaribu kuchambua na kuona kuwa tatizo la kinidhamu kama la Molinga haliwezi kuwa sababu ya kumtema kabisa.
“Molinga ni mchezaji sahihi ambaye anaweza kuingia katika timu moja kwa moja na akafanya vizuri, nimewaomba viongozi kumpa nafasi ili aonyeshe uwezo na nashukuru sana wamenielewa na kumrudisha.
“Kwa staili yake ya uchezaji, huyu ni msaada mkubwa sana kwa Yanga kwani nimegundua ni mzuri sana kwa mipira iliyokufa jambo ambalo ni faida kubwa kwetu. Hivi ninavyokwambia kama ataendelea vizuri mazoezini naweza kumpa nafasi kwenye mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Azam FC,” alisema Eymael ambaye alianza Ligi Kuu Bara kwa kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Kagera Sugar.
Kwa maana hiyo, Molinga ataendelea kufanya mambo akiwa sambamba na mastaa wapya waliosajiliwa kwenye dirisha dogo akiwemo Ditram Nchimbi, Tariq Seif, Yikpe Gnamein na Haruna Niyonzima.

ANAWAJUA AZAM NDANI, Nje
Macho ya wapenzi wa soka wengi yatakuwa yakifatilia mechi ya Azam na Yanga pale Uwanja wa Taifa.
Hata hivyo, Eymeal alisema hana hofu kwa kuwa ameifuatilia vizuri Azam kwani ni shabiki mkubwa wa soka la Afrika hasa nchi za DR Congo, Afrika Kusini, Naigeria, Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania.
“Ili kupata matokeo ninazo video za mechi za Azam na nimekaa na wachezaji wangu kuwaelekeza vile ambavyo wapinzani wetu wanacheza wanapokuwa na mpira na wanapokuwa hawana. Ni jukumu letu kwenda kufanya mambo tuliyokubaliana ili kupata matokeo bora,” alisema.