Duke Abuya asajili miaka miwili Nkana FC

Muktasari:

Mwaka jana, iliripotiwa kuwa, Abuya angejiunga na mabingwa wa kihistoria wa soka la Tanzania, klabu ya Yanga, kabla ya dili hilo kufeli dakika za mwisho.

Nairobi. Kiungo wa Kariobangi Sharks, Duke Abuya amesaini kandarasi ya miaka miwili ya kuichezea Nkana FC, inayoshiriki Ligi Kuu Zambia.

Abuya ameungana na Wakenya wenzake, Harun Shakava, Duncan Otieno na Musa Mohammed, ambao wote wanachezea klabu hiyo, alianza kufanya mazoezi na Nkana FC, juma lililopita na baada ya kuonesha hawakusita kumsajili.

Mchezaji huyo, amekuwa mmoja wa wanaspoti nyota ambao wamekuwa wakifuatiliwa na klabu kadhaa, kwa misimu miwili sasa na zaidi ya mara moja amekuwa akihusishwa kutaka kuigura Kariobangi Sharks, ambayo msimu huu inafanya vibaya kwenye KPL.

Mwaka jana, iliripotiwa kuwa, Abuya angejiunga na mabingwa wa kihistoria wa soka la Tanzania, klabu ya Yanga, kabla ya dili hilo kufeli dakika za mwisho. Mbali na Yanga, mabingwa watetezi wa KPL, Gor Mahia nao walidaiwa kuwa mbioni kutangaza sajili yake.

Abuya, alianzia soka lake katika klabu ya GFC 105, inayoshiriki ligi daraja la kwanza (zamani Nationwide Zone B), ambapo baada ya kuichezea klabu hiyo kwa muda mrefu, alihamia Mathare United, na baadae akatua Sharks.