Dudu Baya kweli mwanangu huna nidhamu

Muktasari:

Dudu Baya amekuwa na tabia ya kucheza na mitandao ya kijamii kwa kujirekodi vipande vya video vya kuwachafua watu

Dar es Salaam. ‘Mwanangu huna nidhamu, mwanangu huna nidhamu… nidhamu nidhamu hata kidogoo… umekuwa huna nidhamu wakubwa uheshimu mtaani umekuwa gumzo na kero kwa walio wengi kila mtu unamuona kinyango kikaragosi….’

Hayo ni baadhi ya mashairi katika wimbo Nidhamu ulioimbwa wa Dudu Baya ambaye leo Januari 7, 2020 amefungiwa kujihusisha na sanaa na Baraza la Sanaa Taifa Basata.

Pamoja na wimbo wa Nidhamu kumjengea heshima kubwa Dudu Baya mwishoni mwa miaka ya tisini, lakini mwenyewe ameshindwa kuishi maisha aliyoyaimba.

Dudu Baya amekuwa ngumi mkononi alianza kwa kumpiga Mr Nice mbele ya mashabiki zake kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee na kufunguliwa kesi katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kwa madai ya kumshambulia mwenzake Mr Nice

Wawili hawa walionyesha kuwa na bifu zito ambalo Dudu Baya akarudia tena kumpiga Mr Nice, jamii ikamlaani akaonekana Dudu Baya kweli, Baadaye akaomba msamaha na kutaka asiitwe tena Dudu Baya bali aitwe Dudu Zuri

Jamii ikasahau mabaya yake, akaimba wimbo wa 'Nimeondoka' kwenye video amevalia mavazi ya nguo yenye rangi nyeupe kudhihirisha kwamba alikuwa mtu mpya.

Akapotea kwenye gemu kabla ya kuibuka tena safari hii akawa mtu wa kuchafua wenzake kwenye mitandao ya kijamii, akawachafua kweli kwa orodha chafu alizokuwa akizitoa za watu maarufu wa kiume wanaojihusisha mapenzi ya jinsia moja.

Dudu Baya alianza kuibuka ghafla mwaka 2018 kupitia kampeni ya Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kupiga vita ushoga jijini Dar es salaam na kuwataka wananchi na wakazi wa jiji hilo kutaja majina kwa siri.

Hapo ndipo Dudu Baya aliamua kutaja kupitia ukurasa wake wa instagram na kujipatia kiki za ghafla zilizomrudisha kwenye ramani, na kutoa wimbo unaoitwa Konki akimshirikisha mwanamuziki Ray vanny kutoka WBC huku akijipachika jina la Konki Master.

Hali hiyo ilimrudisha kwenye chati Dudu Baya hadi mwanamuziki Diamond Platinumz mwaka huo huo 2018 alivyoanzisha Tamasha la Wasafi Festival lilijumuisha wasanii wengi kutumbuiza akiwemo Dudu Baya ndipo ukaribu na Diamond na viongozi wake ulipoanzia

Dudu Baya aliendeleza tabia ya kucheza na mitandao ya kijamii kwa kujirekodi vipande vya video vya kuwachafua watu, hadi ilipofika mwaka jana (2019) Dudu Baya alikamatwa akishutumiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Marehemu Ruge Mutahaba.

Hii ilikuwa ni agizo kutoka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alilitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kumchukulia hatua msanii Tumaini Godfrey maarufu 'Dudu Baya' ambaye alikuwa akimdhihaki Ruge Mutahaba kabla na baada ya kifo chake.

Kitendo cha mwanamuziki huyo kilizua gumzo mitandaoni wengine wakisema anatekeleza uhuru wake wa kutoa maoni yake, lakini wengine wakikemea kitendo hicho wakikiita si cha kiungwana wala kistaarabu.

Baada ya hapo mwaka jana huo huo Dudu Baya akajaribu kuwasahaulisha watu na ubaya huo kwa kuibukia kanisani akidai ameokoka rasmi kwa kufanyiwa ibada na Mtume Boniface Mwamposa ‘Bull Dozer’ wa Kanisa la Inuka Uangaze Kawe jijini Dar es Salaam. Mwanaspoti lilipata kuongea nae Dudu Baya baada ya kutanga kuokoka ambapo alisema maneno haya: “Kwasasa mimi ni mpya, Namshukuru sana Mwamposa kwa kwa kunipa neno la imani”.

Lakini safari hii tena ambapo jana kaibuka kivingine kwa kuwatuhumu Kampuni ya Wasafi Media kuwa walimuweka kikao kuwa aache tabia ya kutukana Serikali na kudai ameambiwa wakae naye mbali, kitendo hiko hajafurahishwa nacho Dudu Baya na kuanza kujirekodi kipande cha video kwa kuwasema Wasafi na Basata.

Basata jana January 6, 2020 likamuandikia barua ya wito msanii huyo kutokana na maneno ambayo amekua akiyazungumza kwenye mitandao ya kijamii ikimtaka Dudu Baya kufika Makao makuu ya Baraza leo Jumanne January 7, 2020 mnamo saa 4 kamili asubuhi,

Dudu Baya mara baada ya kupata taarifa hiyo alijirekodi tena kipande cha video kutupia mtandaoni kilichokuwa kinaonyesha, ameuona wito huo lakini hataenda.

Badala yake amelitaka Baraza hilo kabla ya kumuita inabidi waziweke sawa baadhi ya media ambazo hazielewani wafanyekazi kwa ushirikiano ili muziki uweze kwenda mbele.