MTU WA PWANI: David Molinga aanze tu kupeleka mizigo stendi

Friday January 3 2020

Mwanaspoti-David Molinga-Yanga-Zahera-aanze tu-kupeleka-mizigo stendi

 

By Charles Abel

DAVID Molinga ndiye kinara wa ufungaji katika kikosi cha Yanga kwenye Ligi Kuu  akiwa amepachika mabao manne hadi sasa sawa na Patrick Sibomana.
Hata hivyo, pamoja na mabao yake hayo, kuna uwezekano finyu kwake kuendelea kubakia katika klabu hiyo licha ya mkataba wake kubakiza muda wa miezi sita kumalizika.
Anaweza kutupiwa virago katika dirisha hili dogo la usajili ambalo litafungwa Januari 15 lakini akinusurika hapo, hakuna dalili zozote kuwa atapona katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa mara baada ya msimu huu kumalizika.
Ndoa baina ya na Yanga imekuwa ni ya mashaka tangu mshambuliaji huyo aliposajiliwa mwezi Agosti mwaka jana chini ya mapendekezo ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera.
Ni kama kila upande umekuwa na mashaka na hauamini mwingine jambo ambalo mara nyingi husababiusha usitishwaji wa mikataba kwa klabu zetu na limekuwa ni utamaduni wa kawaida.
Kuna sababu kadhaa ambazo pengine zinaweza kufanya tusimuone Molinga akiwa na jezi za Yanga ndani ya siku au miezi ijayo.
Kitendo cha utovu wa nidhamu ambacho alikionyesha katimu mchezo uliopita dhidi ya Biashara United, kinaweza kuwa petroli ambayo itatumika kumuunguza na kuwa sababu kuu ya kumuondoa mshambuliaji huyo katika kikosi cha Yanga.
Muda mfupi baada ya kutolewa, aliamua kubadilisha nguo na kubaki na mavazi ambayo hayakuwa rasmi kwa timu siku hiyo na mbaya zaidi akalazimisha kukaa kwenye benchi la wachezaji wa akiba kabla ya kuondewa na kulazimika kupanda jukwaani kutazama mechi.
Molinga alifanya hivyo pengine kama ishara ya kuonyesha kuchukizwa kwake na uamuzi wa benchi la ufundi kumpumzisha mwanzoni mwa kipindi pili kumpisha Tariq Seif ambaye ni mshambuliaji aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha hili la usajili akitokea Misri.
Bahati mbaya kwa Molinga ni kwamba, mchezaji aliyeingia badala yake, ndiye aliyeenda kuifungia Yanga bao pekee la ushindi katika mchezo huo jambo ambalo Molinga alishindwa kulifanya kwa dakika 45 za kwanza alizocheza.
Sio mara ya kwanza kwa Molinga kuonyesha kuchukizwa na uamuzi wa benchi la ufundi kumtoa kwani tayari alishawahi kufanya hivyo katika mchezo dhidi JKT Tanzania ambao japo hakufanya kama kile alichokifanya dhidi ya Biashara United, alirusha mikono kama ishara ya kutofurahishwa na uamuzi wa benchi la ufundi.
Lakini kingine ni kwamba Yanga bado inaonekana haina imani na uwezo wa Molinga na ndio maana imejikita kusaka wachezaji wanaocheza nafasi za ushambuliaji katika dirisha hili dogo la usajili wakiamini kwamba mshambuliaji huyo raia wa DR Congo bado sio mtu wa kumtegemea sana katika kufumania nyavu.
Wamemnasa Ditram Nchimbi na Tariq Seif na wametajwa kuwa katika mipango ya kumsajili nyota mwingine wa kigeni. Pamoja na kwamba anafunga mabao, wanamuona Molinga kama mchezaji wa daraja la kawaida ambaye hawezi kuwa tegemeo kwao pale wanapokuwa wamebanwa vilivyo.
Jambo lingine ambalo linaweza kuchangia kumuondoa Molinga ndani ya Yanga ni upepo wa Kocha Zahera ambaye miezi miwili iliyopita alitimuliwa na timu hiyo.
Bado baadhi ya vigogo ndani ya Yanga wanahisi kocha huyo ana kundi fulani la wachezaji waaminifu kwake ambao aliwasajili na wengine marafaiki zake, anaoweza kuwatumia kwa kuwashawishi wacheze chini ya kiwango ili Yanga isifanye vizuri na mmojawapo ni Molinga.
Na Molinga mwenyewe pengine anajiona kama mtoto wa kambo ndani ya klabu hiyo hasa baada ya kocha na rafiki yake wa karibu aliyemleta kikosini, Zahera kutupiwa virago vyake.
Huenda anahisi anafanyiwa mabadiliko kwa kuonewa kisa tu alisajiliwa na Zahera na anadhani anahitaji kucheza kwa dakika nyingi ili kuweza kuisaidia timu.
Kinachoonekana kwa sasa ni kila upande kumtega mwenzake ili usionekane umekosea pindi uamuzi mgumu utakapochukuliwa ama kwa Molinga kuomba mwenyewe kuvunja mkataba au Yanga kuamua kumtema au kutomuongezea mpya pindi huu wa sasa utakapomalizika.
Uamuzi wa Molinga kuvunja mkataba yeye mwenyewe maana yake utainufaisha zaidi Yanga kwa sababu atalazimika kuilipa fidia ya muda ambao umebakiza.
Lakini kama ni Yanga ndio itaamua kuvunja mkataba kwa sasa au kutomuongezea mshambuliaji huyo mara baada ya huu wa sasa kumalizika, ni wazi kwamba faida kubwa itakuwa upande wa Molinga.
Kwanza atajiunga na timu nyingine bure pasipo Yanga kunufaika chochote lakini pia atavuna fedha kutoka kwa Yanga kama fidia ya mkutano wake kuvunjwa.
Molinga anapaswa kuangalia kilicho bora zaidi kwa upande wake kati ya viliivyo tajwa hapo juu. Asijiamini sana kama anaweza kubakia ndani ya kikosi cha Yanga kwa muda mrefu kisa tu anaonyesha uchu wa kutaka kucheza na kuisaidia timu.
Muda na saa yoyote anaweza kuonyeshwa mkono wa kwaheri ni suala la muda tu.

Advertisement