Bongo Zozo amkaribisha Samatta Norwich City

Muktasari:

Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail, Norwich imeripotiwa kuingia katika vita ya kuwania saini ya mshambuliaji huyo mwenye thamani ya  Pauni 10 milion.

MZEE wa Fujo Zisizoumiza, Nick Reynolds ‘Bongo Zozo’ amefurahishwa na tetesi za Norwich kuiwania saini ya mshambuliaji na nahodha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ambaye amekuwa katika kiwango bora na klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji.
Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail, Norwich imeripotiwa kuingia katika vita ya kuwania saini ya mshambuliaji huyo mwenye thamani ya  Pauni 10 milion.
“Nilipokuwa Tanzania nilimweleza kuwa ajiunge na Norwich yaani atakuwa akija nyumbani kula chakula kabisa kabla ya kwenda kuwachakaza huko, sipati picha akicheza na Pukki, nitakuwa nikienda kufanya fujo isiyoumiza,” alisema.
“Sasa itabidi viongozi wa Norwich wafanye kweli wasilete mchezo waweke pesa na kumchukua mapema.”
Samatta mwenye umri wa miaka 27 alikuwa mfungaji bora wa klabu hiyo msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Ubelgiji akifunga magoli 25 na kuisaidia KRC Genk kushinda taji lake la nne la ligi katika historia ya klabu hiyo.
Samatta pia alitawazwa kuwa mshindi wa taji la Ebony Shoe mwaka uliopita ambalo hutolewa kwa mchezaji bora wa mwenye asili ya Afrika nchini Ubelgiji. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Tanzania   awali alikuwa akihusishwa kuwindwa na klabu kadhaa za Uingereza ikiwemo Leicester City, Aston Villa, Watford, West Ham, Everton na Burnley.