Bluefins yatwaa ubingwa kuogelea Morogoro

Muktasari:

Waogeleaji wa wasichana wa klabu hiyo walikusanya jumla ya pointi 1,224 wakati wavulana walikusanya pointi 1,397.

Dar es Salaam. Klabu ya Bluefins ya Dar es Salaam imetwaa ubingwa wa mashindano ya kuogelea ya Morogoro (MIS Piranhas) yaliyomalizika jana Jumapili.

Klabu hiyo imekusanya jumla ya pointi 2,621 na kuzipiku klabu nyingine tatu zilizoshiriki mashindano hayo yaliyofanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Morogoro (MIS).

Nafasi ya pili ilichukuliwa na klabu ya Taliss-IST iliyopata pointi 2,583 wakati Mis Piranhas walimaliza katika nafasi ya tatu kwa kupata pointi 1,914 na Dar Swim Club (DSC) ilipata jumla ya pointi 1907 na kumaliza katika nafasi ya nne.

Ubingwa huo ni wa kwanza kwa klabu hiyo iliyoanzishwa kwa klabu hiyo miaka ya hivi karibuni.

Waogeleaji wa wasichana wa klabu hiyo walikusanya jumla ya pointi 1,224  wakati wavulana walikusanya pointi 1,397.

Muasisi na kocha mkuu wa timu hiyo, Rahim Alidina alisema kuwa ushindi huo umetokana na ushirikiano baina yao na makocha, wazazi, wadau na juhudi za waogeleaji kuiletea sifa klabu yao.

Alidina alisema kuwa mwanga wa mafanikio ulianza mwaka mwaka 2018 baada ya kushinda nafasi ya pili na mwaka jana walishinda pia nafasi ya pili.

“Hapa ndipo tuliona kushika nafasi ya kwanza inawezekana na kuweka lengo mwaka huu, nawapongeza wote waliofanikisha ushindi huu na kuanza mwaka 2020 vizuri,” alisema Alidina.

Waogeleaji wasichana walioleta sifa katika klabu hiyo ni Aliyana Kachra, Zainab Moosajee, Maryam Ipilinga, Alexis Misabo, Aminaz Kachra, Lina Goyayi, Muskan Gaikwad, Filbertha Demello, Niharika Mahapatra, Yumna Hassan na Natalia Ladha.

Waogeleaji wa kiume walioleta sifa ni pamoja na  Mohammad hussein Imran, Kaysan Kachra, Sahal Harunani, Moiz Kaderbhai, Jay Govindji, Raihan Abdullatif, Hassan Harunani, Idris Zavery, Isaac Mukani, Kabeer Lakhani, Salman Yasser, Gervas Sayi na  Delbert Ipilinga.

Pia wamo, Zac Okumu, Adam Patwa, Qais Kanji, Kahil Walli, Christian Fernandes, Avinav Mahapatra, Aaron Akwenda, Shuneal Bharwani, Enrico Barretto, Burhanuddin Gulamhussein na Rayyan Khan.