Bigirimana: Kagere mtamu ila sikubali!

Muktasari:

Kirundi jina Bigirimana lina maana ya kila kitu kinapangwa na Mungu, huku jina lake la kwanza Blaise likiwa ni baraka. Ma amekiri kufaidika na majina hayo kiasi kwamba anajiona ni wa tofauti.

UNAJUA maana ya majina ina athari kubwa kwa wanaoyamiliki? Majina huwa na tija katika maisha ya watu na kama unabisha muulize straika wa Namungo FC, Blaise Bigirimana Babikakule atakupa ushuhuda namna anavyofaidi ‘baraka’ za jina lake.
Kirundi jina Bigirimana lina maana ya kila kitu kinapangwa na Mungu, huku jina lake la kwanza Blaise likiwa ni baraka. Ma amekiri kufaidika na majina hayo kiasi kwamba anajiona ni wa tofauti.
Kati ya faida za jina lake amezitaja kuwa ni kupendwa na watu, muda mwingi ni mwenye furaha na amepata baraka za kimaendeleo ambazo hakutaka kuweka wazi akidai kwamba ni siri yake.
Katika kupiga stori za hapa na pale na Mwanaspoti, Bigirimana amefunguka mengi namna anavyoiona Ligi Kuu msimu huu, changamoto na matarajio yake.

NAFASI YAKE NAMUNGO
Jina la Bigirimana lilianza kujulikana akiwa na Stand United ‘Chama la Wana’ kutokana na uwezo wake uwanjani, lakini baadaye akaenda kujiunga na Alliance na kwa sasa ni mwajiriwa wa Namungo FC. Alipoulizwa  anaionaje nafasi yake ndani ya kikosi cha kwanza cha Namungo FC? Alijibu kuwa kazi iliyomfanya aondoke nchini kwao Burundi na kuja Tanzania ni soka. “Burundi nimeacha ndugu zangu ninaowapenda kwa sababu ya kazi, siwezi kufanya mchezo kabisa, nina asilimia 100 za kucheza ndani ya kikosi cha kwanza, nipo kwa ajili ya kupambana na sio kuonewa huruma,” anasema.

AMKOMALIA KAGERE
Katika mechi saba za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu huu, amefunga mabao mawili tu na kumfanya ndani ya msimu mitatu kuwa na mabao 15, kwani misimu miwili iliyopita alifunga mabao 13 akiwa na timu za Stand na Alliance.
Alipoulizwa anaona nani ana nafasi ya kuchukua kiatu cha dhahabu msimu huu? Haya ndio majibu yake: “Siwezi kuwa mtabiri, yeyote anaweza akachukua kiatu ndio maana ya ushindani, huwezi kumnyoshea mikono Meddie Kagere kisa anaongoza kwa mabao tisa, tutapambana mpaka mwisho.
“Maadam muda upo na mechi bado ni nyingi naamini kabisa nikikomaa naweza kuyafikia mabao tisa na kuyapita.”

ANAIONAJE LIGI?
Kama kuna changamoto anaiona kwenye Ligi Kuu ni kusimama kwa muda mrefu kitu anachoona kinapunguza msisimko wa ushindani.
“Ligi inaposimama kuna ladha inakuwa inapungua baadaye ikiendelea mnakuwa kama mnawakumbusha watu kwamba kuna ligi, binafsi naona sio nzuri sana,” anasema.
Mbali na hilo, anasema anauona ni msimu wa mchezaji kuonyesha ufundi wake kutokana na mechi kuwa nyingi, akiamini inawapa nafasi ya kupata uzoefu.
“Unapocheza mechi nyingi unakuwa unaonyesha ufundi, pia unapata uzoefu na kujiamini, hivyo naona ina faida kwa mchezaji,” anasema.
Pamoja na hilo, anasema ushindani uliopo kwenye ligi unawafanya wawe makini kushinda kila mechi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo.

MALENGO YAKE
Anasema anatamani kuandika rekodi ya aina yake itakayoonyesha ubunifu wake kwenye kazi zake: “Napenda kuwa na jipya, inawezekana kikubwa pumzi, bidii na nidhamu ya kazi vipo ndani ya uwezo wangu.”