Basata yamfungia Dudubaya kutojihusisha na sanaa

Muktasari:

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limemfutia usajili msanii wa Bongofleva Tanzania, Dudubaya kutojohusisha na shughuli zozote za sanaa baada ya kukataa wito wa Baraza hilo.

Dar es Salaam.Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limemfutia usajili msanii wa Bongofleva Tanzania, Dudubaya kutojohusisha na shughuli zozote za sanaa.

Tamko hilo limotolewa leo Januari 7, 2020 na Katibu Mtendaji, wa baraza hilo, Godfrey Mngereza baada ya msanii huyo kukaidi wito wao wa kumtaka aende ofisini kwao kwa ajili ya mahojiano.

Dudubaya ambaye jina lake halisi ni Godfrey Tumaini, alitakiwa kufika ofisi za Basata leo Januari 7, 2020 saa 4:00 asubuhi baada ya kusambaa kwa video zake kwenye mitandao ya kijamii akizungumzia mambo mbalimbali, ambapo Basata imeeleza ametumia kauli zisizokuwa na maadili wala staha.

Hata hivyo Dudubaya aliukataa wito huo kwa kulijibu Baraza hilo kuhangaikia kwanza na migogoro iliyopo kati ya baadhi ya vyombo vya habari na wasanii ili kuufanya muziki usonge mbele huku maneno aliyoyatumia katika video zake akieleza kuwa ni ya kawaida.

Kutokana na kutoitikia wito huo, Mngereza katika tamko lake hilo amesema baraza limechukua hatua ya kumfutia usajili wake kuanzia leo Januari 7, 2020.

"Kwa mantiki hii Basata halitavumilia wasanii wachache ambao wanataka kuigeuza sekta ya sanaa kwa kutumia lugha chafu na isiyo na staha mbele ya jamii.

"Pia baraza linatoa onyo kwa taasisi, kampuni na mtu yeyote kutofanya kazi ya sanaa na msanii huyu," amesema Mngereza.

Katibu huyo amewakumbusha wasanii na wadau wote wa sanaa nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta ya sanaa nchini pamoja na kuzingatia sheria za nchi.